Wairani 85,200 kwenda kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46408
Wairani 85,200 wanatazamiwa kwenda nchini Saudi Arabia kutekeleza ibada tukufu ya Hija mwaka huu.
(last modified 2025-06-15T08:05:10+00:00 )
Jun 28, 2018 03:48 UTC
  • Wairani 85,200 kwenda kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu

Wairani 85,200 wanatazamiwa kwenda nchini Saudi Arabia kutekeleza ibada tukufu ya Hija mwaka huu.

Hamid Mohammadi, Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara la Iran aliyasema hayo jana Jumatano na kuongeza kuwa, ndege za kuelekea mji mtukufu wa Madina zitaanza kuondoka hapa nchini Julai 18 huku zile zinazoelekea mjini Jiddah zikitazamiwa kuanza kuondoka Julai 30.

Amesema hatua zote zimechukuliwa kwa ajili ya maandalizi ya safari hizo na nguzo hiyo ya Kiislamu, yakiwemo masuala ya malazi, huduma za afya na chakula.

Februari mwaka huu, Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija na Ziara, Hujjatul Islam wal Muslimin Ali Qadhi Asghar alisema kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia zimetiliana saini mapatano na kwa mujibu wa mwafaka huo, mbali na kudumishwa suhula za Mahujaji za mwaka jana, mwaka huu pia kutakuwa na huduma bora zaidi."

Iran imekuwa ikisisitizia umuhimu wa kudhaminiwa usalama Mahujaji wake

Mwenyekiti wa Shirika la Hija la Iran, Hamid Mohammadi na Waziri wa Hija wa Saudia Mohammad Saleh bin Taher Benten walifanya mazungumzo Disemba mwaka jana kwa lengo la kuandaa ratiba ya Hija ya mwaka huu.

Ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo ulisisitiza ulazima wa kupewa huduma bora na kudhaminiwa usalama sambamba na kuhifadhi heshima ya Mahujaji Wairani.