Qassemi: Iran haijapokea pendekezo la JCPOA kutoka Umoja wa Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46475-qassemi_iran_haijapokea_pendekezo_la_jcpoa_kutoka_umoja_wa_ulaya
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria habari kuwa Umoja wa Ulaya umewasilisha pendekezo la kuunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, (JCPOA), na kusema, "hadi sasa Iran haijapokea kifurushi cha mapendekezo kutoka Umoja wa Ulaya."
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 30, 2018 11:44 UTC
  • Qassemi: Iran haijapokea pendekezo la JCPOA kutoka Umoja wa Ulaya

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria habari kuwa Umoja wa Ulaya umewasilisha pendekezo la kuunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, (JCPOA), na kusema, "hadi sasa Iran haijapokea kifurushi cha mapendekezo kutoka Umoja wa Ulaya."

Baadhi ya vyombo vya habari leo vimemnukulu mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini akisema kuwa viongozi wa umoja huo wameidhinisha kifurishi cha kuunga mkono JCPOA ili kudhamini maslahi ya Iran. Qassemi amesema Iran itapokea kifurishi hicho cha mapendekezo katika kipindi cha siku mbili zijazo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa: "Nchi za Umoja wa Ulaya hivi sasa zinaendeleza mazungumzo ya mwisho kuhusu kuwasilisha pendekezo hilo kwa Iran na kwamba pindi Tehran itakapolipokea pendekezo hilo italichunguza."

Qassemi amesema Iran itachunguza kwa kina kifurishi cha mapendekezo  kwa maslahi ya taifa na kisha itachukua maamuzi kuhusu iwapo itabakia au itajiondoa katika JCPOA.

Mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya Federica Mogherini

Itakumbukwa kuwa Mei 8 mwaka huu, Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuindoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha wakati wa urais wa Barack Obama.

Nchi zingine tano zilizoafiki mapatano ya JCPOA, zikiwemo za Ulaya zimesisitiza kuwa zitabakia katika mapatano hayo ya Vienna.

Kwa kuzingatia historia hasi ya Umoja wa Ulaya katika kukiuka ahadi zake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alitoa masharti kadhaa kwa umoja huo katika mapatano hayo ya nyuklia. Miongoni mwa masharti hayo ni kutojadiliwa suala la makombora ya Iran, uwepo wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati, EU kutakiwa kununua mafuta ya Iran kwa kiwango kinachotakiwa, kuwepo uhusiano wa kibenki kati ya Iran na Umoja wa Ulaya na umoja huo kupinga wazi vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hili.