Iran: Washauri wetu wa kijeshi kusalia Syria kuzima chokochoko za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46647-iran_washauri_wetu_wa_kijeshi_kusalia_syria_kuzima_chokochoko_za_israel
Mshauri wa Masuala ya Kimataifa wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, washauri wa kijeshi wa Iran watasalia nchini Syria kuisaidia nchi hiyo ya Kiarabu kuzima chokochoko za mabaki ya magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi ajinabi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2018 09:41 UTC
  • Iran: Washauri wetu wa kijeshi kusalia Syria kuzima chokochoko za Israel

Mshauri wa Masuala ya Kimataifa wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, washauri wa kijeshi wa Iran watasalia nchini Syria kuisaidia nchi hiyo ya Kiarabu kuzima chokochoko za mabaki ya magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi ajinabi.

Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Salah al-Zawawi, Balozi wa Palestina mjini Tehran na kubainisha kuwa, "Utawala wa Kizayuni unajaribu kueneza satua yake nchini Syria baada ya kusambaratishwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS), lakini vikosi vya muqawama na washauri wa kijeshi wa Iran wataendelea kushirikiana na serikali ya Syria kuzima njama hizo za magaidi."

Amesisitiza kuwa, katu wananchi wa Syria hawatouruhusu utawala haramu wa Israel uendelee kuwepo katika ardhi yao, baada ya kusambaratishwa genge la kigaidi la Daesh. 

Abdollahian ameongeza kuwa,  hakuna mafanikio yoyote iliyoyapata Marekani wala utawala bandia wa Israel katika madai yao ya kupambana na magenge ya kigaidi nchini Syria, bali hata wamekuwa wakiwasaidia viongozi wakubwa wa genge la Daesh kutoroka katika maeneo wanakozidiwa nguvu. 

Magaidi wanaoungwa mkono na Wamagharibi nchini Syria

Mgogoro wa kubuniwa na madola ya Magharibi na washirika wao wa Kiarabu nchini Syria uliibuka mwaka 2011 ambapo madola hayo yaliwatuma wanachama wa makundi ya kigaidi kwa ajili ya kuvuruga hali ya mambo sio tu katika nchi hiyo ya Kiarabu, bali katika eneo hili kwa ujumla, kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni.

Kufuatia hali hiyo serikali halali ya Rais Bashar al-Assad iliomba msaada kutoka kwa Iran kwa ajili ya kupambana na makundi hayo ya kigaidi na ukufurishaji.