Zarif: JCPOA imethibitisha Marekani haiaminiki hata kidogo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akizungumza kwa munasaba wa kufikiwa mapatano ya nyuklia maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA, baina ya Iran madola sita makubwa ya kundi la 5+1 amesema: 'JCPOA imethibitisha kuwa serikali ya Marekani haiwezi kuaminika hata kidogo."
Itakumbukwa kuwa Julai 14 mwaka 2015, mapatano ya nyuklia ya Iran, JCPOA, yalifikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 ambalo lilijumuisha Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Marekani na Ujerumani. Mapatano yalifikiwa baada ya mazungumzo magumu na ya miaka kadhaa lakini hata baada ya kuyaafiki, Marekani ilikengeuka na kuchukua uamuzi wa upande mmoja mwezi Mei mwaka huu na kujiondoa katika maptano hayo ya kimataifa.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika ujumbe kwa njia ya Twitter siku ya Jumamosi ameandika hivi: "Katika hali ambayo Iran ilifahamu fika kuwa Marekani si nchi ya kuaminika sasa waitifaki wa Washington nao wamefahamu suala hili. JCPOA imethibitisha kuwa serikali ya Donald Trump haiwezi kuaminika hata kidogo."

Zarif ameongeza kwamba, licha ya hatua hiyo ya Marekani, JCPOA katika mwaka wake wa tatu inabakia kuwa ushindi wa kidiplomasia wa pande kadhaa.
Baada ya Marekani kujiondoa JCPOA na kufuatia ombi la nchi za Ulaya la kutaka JCPOA ilindwe, Iran iliafiki kuzipa fursa mpya nchi hizo za Ulaya ili ziweze kudhamini maslahi ya Iran kivitendo wakati wa kurejea vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Mazungumzo kuhusu kadhia hiyo yangalia yanaendelea.