Iran yaitaka EU iache maneneo matupu na kutekeleza ahadi kivitendo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i46861-iran_yaitaka_eu_iache_maneneo_matupu_na_kutekeleza_ahadi_kivitendo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sambamba na kusisitiza umuhimu wa uhusiano wa Iran na Umoja wa Ulaya baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, amesema, baada ya Ulaya kuahidi kufungamana na JCPOA, sasa umewadia wakati wa kutekeleza ahadi hizo kivitendo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2018 08:34 UTC
  •  Iran yaitaka EU iache maneneo matupu na kutekeleza ahadi kivitendo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sambamba na kusisitiza umuhimu wa uhusiano wa Iran na Umoja wa Ulaya baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, amesema, baada ya Ulaya kuahidi kufungamana na JCPOA, sasa umewadia wakati wa kutekeleza ahadi hizo kivitendo.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano yake na Televisheni ya Euronews na kuongeza kuwa, nchi za Ulaya hazipaswi kutosheka na kutoa taarifa kwani Iran sasa inataka kuona njia za kivitendo hasa kuhusu miamala ya kibenki, uwekezaji, nishati, uchukuzi na kuunga mkono mashirika ya wastani na madogo ya kibishara ya Ulaya ambayo yanataka kufanya biashara na Iran.

Kuhusiana na mkutano wa hivi karibuni wa marais Vladimir Putin wa Russia na Donald Trump wa Marekani huko Helsinki, Finland, na sisitizo lao kuhusu ushirikiano katika kadhia ya mgogoro wa Syria, Zarif amesema:"Hatima ya Syria inapaswa kuamuliwa na Wasyria wenyewe." Ameongeza kuwa hadi sasa Wasyria wameweza kustahamili mashinikizo mengi ya magaidi, wavamizi na wenye misimamo mikali.

Zarif ameongeza kuwa, Iran imedumisha ushirikiano mzuri na Russia pamoja na serikali ya Syria na itaendelea kufanya hivyo na kwamba lengo la pande tatu ni kupambana na ugaidi pamoja na misimamo mikali.

Aidha ameashiria njama za Marekani na waitifaki wake za kuyanga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria na kusema: "Matamshi ya Trump kuwa Iran haipaswi kunufaika na kushindwa kundi la ISIS (Daesh) ni thibitisho kuwa Rais wa Marekani anaunga mkono kundi la kigaidi la ISIS."