Siddiqui: Iran haitafanya mazungumzo na serikali na rais wa sasa Marekani
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo mjini Tehran amesema Wamarekani si watu wa kufanya nao mazungumzo na iwapo kuna siku Iran itafanya mazungumzo basi si na rais na serikali ya sasa ya Marekani.
Hujjatul Islam Kadhim Siddiqui khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran ameashiria pendekezo la Rais wa Marekani la kufanya mazungumzo bila masharti na viongozi wa Iran na kusema kujiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA kumeondoa uwezekano wa kufanya mazungumzo na serikali ya sasa ya Marekani.
Akizungumza katika mkutano na waandishi habari Jumatatu iliyopita Trump alijibu swali kuhusu uwezekano wa kufanya mazungumzo na Iran na kudai kuwa: 'Wakati wowote ule' na 'bila masharti yoyote' niko tayari kufanya mazungumzo na wakuu wa Iran.'
Rais wa Marekani anahadaa umma kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hali ambayo Mei 8, alikariri madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran na kutoa tangaza la kuondoka nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha vikwazo vipya.

Sheikh Siddiquie ameashiria mnasaba wa Agosti 5 ambayo ni 'Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu' na kusema: Baadhi ya nchi zinadai kutetea haki za binaadamu huku zikiunga mkono mashambulizi ya mabomu ya kemikali na kuuawa watu wasio na hatia. Amesema haki za binadamu katika Uislamu ndio haki halisi za binadamu.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran pia ameashiria ushindi wa majeshi ya Syria na Yemen katika vita dhidi ya magaidi na kusema ushindi huo unaashiria kushindwa Marekani na utawala haramu wa Israel. Ameongeza kuwa hivi karibuni magaidi wanaopata himaya ya Saudi Arabia watapata pigo la mwisho.