Ayatullah Khatami: Marekani na waitifaki wake watapata hasara katika vita na Iran
Khatibu wa Sala ya Idul Adha mjini Tehran amesema Marekani inafahamu kuwa, iwapo kutajiri vita baina yake na Iran, si tu kuwa binafsi itapata hasara, bali pia muitifaki wake mkuu yaani, utawala wa Kizayuni wa Israel nao pia utapata pigo kubwa.
Ayatullah Ahmad Khatami ameyasema hayo leo Jumatano asubuhi katika hotuba zake za Sala ya Idul Adha mjini Tehran na kuongeza Marekani inapaswa kufahamu iwapo italidhuru hata kidogo taifa la Iran basi itadhalilishwa na Wairani.
Khatibu wa Sala ya Idul Adha mjini Tehran ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka 40 sasa tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran limeweza kuwafanya maadui wapoteze matumaini. Ameongeza kuwa, stratijia ya adui katika hali ya sasa ni kuibua mifarakano baina ya Waislamu. Ameongeza kuwa, moja ya stratijia za maadui ni kuhakikisha kuwa Waislamu halisi na wanaofuata njia ya haki wanauawa kwa umati.
Ayatullah Khatami ameashiria matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu kutofanya mazungumzo na Marekani na kusema: "Tokea mwanzo wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa, Marekani imekuwa ikitaka kufanya mazungumzo na wakuu wa Iran lakini haikufanikiwa na itaangamia kaburini na ndoto yake hiyo ya kutaka kufanya mazungumzo na Iran."

Khatibu wa Sala ya Idul Adha mjini Tehran ameendelea kusema kuwa, kile ambacho Marekani inataka si mazungumzo bali inataka udikteta katika mazungumzo. Amesema Marekani inataka mazungumzo kuhusu upunguzaji ushawishi wa Iran katika eneo na pia kupunguza uwezo wa makombora ya kujihamu ya Iran. Ayatullah Khatami amesema maadui wanapaswa kufahamu kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itasimama kidete mbele ya udikteta.