Iran yatuma salamu za rambirambi kwa Tanzania kufuatia ajali ya kivuko, Mwanza
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametuma salamu za rambirambi kwa taifa na serikali ya Tanzania kufuatia ajali ya kuzama kivuko cha MV Nyerere katika ziwa Vctoria huko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Bahram Qassemi amesema Iran inasikitishwa sana na ajali hiyo iliyosababisha vifo vya idadi kubwa ya watu. Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa taifa na serikali ya Tanzania na vilevile kwa familia za watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Kivuko cha MV Nyerere kilizama jana mchana wakati kilipokuwa kikielekea kisiwa cha Ukara kutoka Bugorara katika Ziwa Victoria wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Tanzania. Idadi kamili ya abiria waliokuwa kwenye kivuko hicho bado haijajulikana lakini baadhi ya habari zinasema kwamba zaidi ya watu 400 walikuwemo katika chombo hicho.
Kivuko hicho kimezama umbali wa mita 50 kabla ya kutia nanga katika kisiwa cha Ukara.
Kivuko cha MV Nyerere kina uwezo wa kubeba abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu.
Rais John Magufuli wa Tanzania amewataka watu wa nchi hiyo kuwa watulivu wakati zoezi la uokoaji likiendelea na ametangaza siku tatu za maombolezo ya taifa kufuatia ajali hiyo.
Hadi kufikia sasa miili ya watu 364 ilikuwa imeopolewa majini na inasadikiwa kuwa wengine wengi wamefariki dunia katika ajali hiyo inayotambuliwa kuwa miongoni mwa ajali mbaya zaidi za majini nchini Tanzania. Wakati huo huo Afisa wa ngazi ya juu wa polisi nchini Tanzania amesema kuwa watu wasiopungua 136 wamepoteza maisha hadi hivi sasa.
Tanzania ina historia ya ajali za vivuko kuzama, mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa ilikuwa ile ya Mei 1996, wakati MV Bukoba kilipozama katika ziwa hilo la Victoria magharibi mwa Tanzania na kusababisha vifo vya karibu watu 1000.