Oct 02, 2018 08:13 UTC
  • Zarif: Iran haitapoteza muda kufanya mazungumzo na US

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran katu haitafanya mazungumzo na Marekani madhali Washington itaendelea kukataa kukumbatia uhalisia wa mambo na muamana.

Katika mahojiano na gazeti la The New Yorker, Mohammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu haiondoi mezani uwezekano wa kufanya mazungumzo na Marekani, lakini hilo linawezekana tu iwapo Washington itaheshimu masharti kadhaa, kubwa zaidi uwepo wa hali ya kuaminiana.

Amefafanua kuwa, "Muamana ni jambo muhimu, na huko ni kutekeleza yale mliyokubaliana." Zarif amebainisha kuwa, msingi wa uhusiano wa kimataifa ni kuheshimu mapatano, vinginevyo mambo yote huporomoka.

Trump dhidi ya dunia

Ifahamike kuwa, mnamo tarehe 8 Mei mwaka huu, Rais wa Marekani Donald Trump alijichukulia uamuzi wa upande mmoja na kukiuka majukumu ambayo nchi yake ilipaswa kuyatekeleza katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa kutangaza kujitoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa.

Baada ya kuchukua hatua hiyo, serikali ya Washington imeanzisha kampeni za kila upande za mashinikizo dhidi ya Iran huku ikitumia kila njia kuzishawishi nchi nyingine ziunge mkono vikwazo vyake vya upande mmoja dhidi ya Tehran.

Tags