Russia yasisitiza, Iran ina mchango mkubwa katika kupambana na ugaidi
-
Sergey Vershinin
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, askari wa Iran wana mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi nchini Syria.
Sergey Vershinin ambaye alikuwa akizungumzia hasira ya utawala wa Kizayuni wa Israel inayotokana na kuwepo washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria amesema kuwa, wanajeshi wa Iran wako nchini humo kutokana na mwaliko rasmi wa serikali ya Damascus.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa, suala hili limesemwa mara nyingi na kuna udharura wa kulikariri kutokana na umuhimu wake.
Kuhusu njama zinazofanywa na baadhi ya nchi za Magharibi za kutaka kuituhumu serikali ya Syria kuwa imetumia silaha za kemikali dhidi ya raia, Sergey Vershinin amesema Moscow imezitahadharisha pande zote hasimu juu ya propaganda chafu zinazofanywa dhidi ya Syria na Russia kuhusiana na kadhia ya Idbil.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, jeshi la serikali ya Syria likisaidiwa na washauri wa kijeshi wa Iran na himaya ya Russia, limefanikiwa kufunga kabisa faili la kundi la kigaidi la Daesh nchini humo. Madola ya Magharibi na mengine ya Kiarabu kama Marekani, dola haramu la Israel na Saudi Arabia zimekasirishwa sana na ushindi wa jeshi la Syria na waitifaki wake dhidi ya magaidi hao.