Kiongozi Muadhamu: 'Iraq yenye nguvu na tulivu' isimame kidete mbele ya maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49579-kiongozi_muadhamu_'iraq_yenye_nguvu_na_tulivu'_isimame_kidete_mbele_ya_maadui
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei leo amekutana na Rais Barham Ahmed Salih wa Iraq hapa mjini Tehran na kusema kuwa, njia ya kuvuka matatizo na kukabiliana na njama za wasiotaka mema ni kulinda umoja wa kitaifa wa Iraq, kuwafahamu vizuri marafiki na maadui na kusimama kidete mbele ya adui sambamba na kuwategemea vijana na kulinda na kuimarisha mahusiano na umarjaiya au wanazuoni wa kidini.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Nov 17, 2018 16:43 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: 'Iraq yenye nguvu na tulivu' isimame kidete mbele ya maadui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei leo amekutana na Rais Barham Ahmed Salih wa Iraq hapa mjini Tehran na kusema kuwa, njia ya kuvuka matatizo na kukabiliana na njama za wasiotaka mema ni kulinda umoja wa kitaifa wa Iraq, kuwafahamu vizuri marafiki na maadui na kusimama kidete mbele ya adui sambamba na kuwategemea vijana na kulinda na kuimarisha mahusiano na umarjaiya au wanazuoni wa kidini.

Ayatullah Khamenei amebainisha furaha yake kutokana na kufanyika kwa mafanikio uchaguzi wa bunge nchini Iraq na baada ya hapo kuchaguliwa rais na waziri mkuu pamoja na maafisa wengine wa nchi hiyo na hivyo kuleta utulivu nchini humo. Ameendelea kusema kuwa,  baada ya duru za udikteta, hivi sasa Wairaqi wanamiliki nchi yao na wana uhuru wa kuchagua viongozi wao. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, baadhi ya serikali na nchi zisizoitakia Iraq mema zinataka Wairaqi wasionje utamu wa ushindi na mafanukio yao makubwa na wanachotaka wao ni kukosekana utulivu nchini humo na katika eneo hili zima.

Mkutano wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Rais wa Iraq

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, njia pekee ya kukabiliana na njama hizi ni kulinda na kuimarisha umoja miongoni mwa makundi ya Wairaqi ni sawa tu wawe Waarabu au Wakurdi au Mashia au Masunni.

Aidha amesema kumfahamu kwa njia sahihi rafiki na adui ni muhimu sana katika sera za kigeni na kuongeza kuwa, baadhi ya serikali za eneo hili na nje ya eneo zina chuki kubwa sana dhidi ya Uislamu, Ushia, Usunni na nchi ya Iraq, hivyo zinaingilia masuala ya ndani ya Iraq. Amesema, kuna haja ya kusimama kidete na kwa uwazi kupambana na adui muovu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wana azma imara ya kuimarisha uhusiano na Iraq na kuongeza kuwa, yeye binafsi ana imani na suala hilo. Amesema: "Iraq azizi, yenye nguvu, yenye kujitegemea na iliyostawi ni yenye faida kubwa kwa Iran na sisi tutabaki pamoja na ndugu zetu Wairaqi."

Ayatullah Khamenei aidha ameashiria kushiriki wafanyaziara Wairani wapatao milioni mbili katika matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS mwaka huu na kusema kuwa, nyoyo za Wairani waliorejea nyumbani kutoka kwenye matembezi hayo zilijaa shukrani kutokana na ukarimu wa watu wa Iraq.