Jitihada za nchi za Umoja wa Ulaya katika kulinda JCPOA
(last modified Mon, 19 Nov 2018 13:02:23 GMT )
Nov 19, 2018 13:02 UTC
  • Jitihada za nchi za Umoja wa Ulaya katika kulinda JCPOA

Katika mwendelezo wa jitihada za nchi za Ulaya za kulinda mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, (JCPOA) Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Jeremy Hunt leo amefika mjini Tehran na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Iran.

Miongoni mwa mada kuu zilizojadiliwa katika mazungumzo hayo ni 'Njia Maalumu ya Kifedha' (SPV) ya nchi za Ulaya ambayo itatoa dhamana ya kulinda maslahi ya kiuchumi ya Iran kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Mazungumo hayo pia yamejadili njia zinginezo za kulinda maslahi ya Iran.

Baada ya Marekani kuanzisha duru ya pili ya vikwazo dhidi ya Iran mapema mwezi huu wa Novemba, nchi za Ulaya zimeendeleza jitihada za kulinda makubaliano ya JCPOA.

Kufuatia hatua ya upande moja ya Marekani ya kujiondoa katika JCPOA na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, wakuu wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakisisitiza udharura wa kulindwa mapatano hayo ya nyuklia na maslahi ya pande mbili. Kwa mtazamo wa wakuu wa Umoja wa Ulaya, kulinda mapatano hayo ya nyuklia ni mafanikio muhimu katika uga wa kulinda amani na usalama wa kimataifa.

Katika upande wa pili, kulinda maslahi ya kiuchumu na kuendeleza mabadilishano ya kibiashara ni maudhui muhimu ambazo zimekuwa zikifuatiliwa na wakuu wa Ulaya. Kuhusiana na suala hilo, Umoja wa Ulaya hivi karibuni ulipitisha sheria ya kuyahami mashirika ya Iran na Ulaya yanayoshirikiana kibishara ili yasidhuriwe na vikwazo vya Marekani. Aidha nchi za Umoja wa Ulaya zimewasilisha 'Njia Maalumu ya Kifedha' (SPV) kwa lengo la kufanya biashara na Iran. Mfumo wa SPV kinyume na mfumo wa SWIFT ambao hutumiwa na benki kote duniani, utakuwa ukitumiwa tu na benki za nchi za Ulaya na hivyo Marekani haitaweza kufuatilia mabadilishano ya kifedha katika mfumo huo. Aidha  sarafu ya dola ya Marekani haitatumika katika mfumo wa SPV na malipo yote yatafanyika kwa sarafu ya Euro ili kukwepa vikwazo vya Marekani kwa wale wanaofanya biashara na Iran.

Pande zilizosalia katika JCPOA baada ya Marekani kujiondoa

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya amefafanua nukta hiyo kwa kusema: "Tutajitahidi kadiri ya uwezo wetu ili Iran iendelee kubakia katika mapatano ya nyuklia na ili watu wa Iran waweze kunufaika kiuchumi na mapatano hayo."

Kulinda misimamo huru ya Ulaya na sisitizo la kuendelea sera za pande kadhaa katika maamuzi ya kimataifa ni malengo mengine ya Umoja wa Ulaya katika kulinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Gerhard Küntzle Balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa anafafanua kuhusu nukta hii kwa kusema: "Kulinda na kuinua kiwango cha kuhuisha sera za pande kadhaa katika masuala ya kimataifa mbele ya sera za maamuzi ya upande moja za Marekani na pia kudumishwa sheria za kimataifa ni kati ya misingi ya sera za kigeni za Ujerumani.

Jitihada za wakuu wa Umoja wa Ulaya za kulinda JCPOA zinafanyika katika fremu ya kudhamini maslahi ya pande mbili na pia kuthibitisha kufungamana kwake na makubaliano hayo ya nyuklia. Jitihada hizo zinaendelea wakati ambao wakuu wa Iran nao pia wamesisitiza udharura wa kufungamana nchi hii na makubaliano ya JCPOA. Wakala wa Umoja wa Mataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) pia nao umethibitisha mara kadhaa kwamba Iran imeheshimu na kutekeleza kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Kwa kuzingatia hayo yote viongozi wa Iran wanataka nchi za Ulaya zichukue maamuzi ya haraka na ya kivitendo.

Federica Mogherini, mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, ni lazima watu wa Iran wapate faida za kuwa katika JCPOA na kuongeza kuwa: "Nchi za Ulaya zina jukumu la moja kwa moja la kuchukua hatua za kivitendo za kulinda makubaliano ya JCPOA."

Hivi sasa wakuu wa Ulaya wanajitahidi kutumia fursa zote zilizop0 ili kulinda JCPOA. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Jeremy Hunt ameitembelea Iran kufanya mazungumzo juu ya suala la kuanzishwa Njia Maalumu ya Kifedha' (SPV) kwa ajili ya nchi za Ulaya kufanya biashara na Iran. Vilevile Helga Schmid Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya pia amefanya mazungumzo na wakuu wa nchi tatu za Ulaya kuhusu suala hilo hilo.

Tags