Mapatano ya JCPOA yanatosha; Iran haitozungumza tena na Marekani
Dk. Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu juhudi za Marekani za kutaka kuanzisha mazungumzo mapya na Iran kwa kusema kuwa, mapatano yaliyofikiwa ya JCPOA ni makubaliano mazuri na kwamba Iran haitofanya tena mazungumzo na Marekani kuhusu miradi yake ya nyuklia.
Zarif alisema hayo Alkhamisi kwenye kikao cha mazungumzo ya Mediterranean mjini Rome Italia na kuongeza kuwa, watu wote wanatambua kwamba sisi ni watu wa mazungumzo na kushirikiana na wengine, lakini wakati linapofika suala la uhuru wa Iran, basi bila ya shaka yoyote tutalinda uhuru wetu na kuachana na ushirikiano ambao thamani yake ni kupoteza uhuru huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesema, kamwe Tehran haiwezi kukubali kufanyiwa ubeberu na kubainisha kuwa: Kwa nini (Marekani) inaitaka Iran ibadilishe siasa zake katika eneo hili? Hivi kwani ni Iran ndiyo iliyomuunga mkono Saddam? Au kwani ni Iran ndiyo inayounga mkono magenge kama ya Daesh (ISIS), Taleban na Jabhatun Nusra? Je, ni Iran ndiyo iliyofanya mashambulio ya Septemba 11 huko Marekani? Hivi kwani ni Iran ndiyo iliyoiwekea vikwazo na kuizingira Qatar? Hivi kwani ni Iran ndiyo inayowashambulia kwa mabomu wananchi wa Yemen? Ukweli wa mambo ni kuwa, ni watu wengine ndio wanaopaswa kubadilisha siasa zao katika eneo la Mashariki ya Kati, si Iran.
Mapatano ya nyuklia ya JCPOA ni matunda ya mazungumzo ya miaka 12 baina ya Iran na Magharibi na yalifikiwa mwaka 2015 kupitia mazungumzo yaliyojulikana kwa jina maarufu la mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1. Wakati huo rais wa Marekani alikuwa ni Barack Obama. Lakini baada ya Donald Trump kuwa rais wa Marekani aliamua kuitoa nchi hiyo kwenye mapatano hayo hapo tarehe 8 Mei mwaka huu wa 2018.
Pamoja na kujitoa Marekani katika mapatano hayo, Iran imeendelea kuyaheshimu na nchi za Ulaya nazo hadi hivi sasa zimekuwa zikitangaza kuyaheshimu mapatano hayo kama ambavyo zinatilia mkazo pia kuendelea kushirikiana na Iran chini ya makubaliano hayo. Msimamo huo wa nchi za Ulaya ni tangazo la wazi la kupinga kwao siasa za upande mmoja za Marekani. Ukweli wa mambo ni kuwa tangu alipoingia madarakani huko Marekani, Donald Trump amekuwa akijitoa kwenye makubaliano mbalimbali ya kimataifa, si ya JCPOA pekee, bali pia makubaliano ya kulinda hali ya hewa yaliyofikiwa mjini Paris Ufaransa na mapatano mengine ya kimataifa; chini ya kaulimbiu yake ya "Marekani Kwanza."
Ukweli wa mambo ni kuwa, ni siasa hizo za Marekani ndizo zinazohatarisha msingi wa ushirikiano wa kimataifa. Hassan Mosaviyan, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anaamini kuwa: Nguvu za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla zinazidi kufifia na ndio maana timu ya hivi sasa ya White House inayoongozwa na Donald Trump inapigania kurejesha mabavu ya Marekani kupitia sera ya kukandamiza madola yote mengine.
Amma swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni kwa nini Trump amezuka na fikra ya kufanya mazungumzo mengine na Iran. Mara kwa mara Trump amekuwa akizungumzia ndoto yake kwamba kuna siku lazima Wairan watakwenda kumuomba afanye nao mazungumzo. Hata hivyo viongozi wa Iran wamekuwa wakisema waziwazi kuwa ndoto hiyo ya Trump kamwe haitoaguliwa.
Kusema kweli lengo la Trump la kutaka kufanya mazungumzo mapya na Iran ni kujaribu kuwaonesha walimwengu kuwa ameweza kuishinikiza Iran mpaka imekubali kufanya mazungumzo naye, kama ambavyo pia anataka kuifanya Iran iachane na misimamo yake ya dhati na kuipunguzia nguvu zake za kiulinzi, jambo ambalo wataalamu wa mambo wanasema, kamwe halitatokea. Sisitizo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika kikao hicho cha Rome, kwamba Tehran kamwe haitofanya mazungumzo mengine na Marekani kuhusu nyuklia ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo.