Jitihada za ulaya za kulinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA
(last modified Thu, 29 Nov 2018 03:05:20 GMT )
Nov 29, 2018 03:05 UTC
  • Jitihada za ulaya za kulinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA, ambayo yalifikiwa Julai mwaka 2015 baina ya Iran na kundi la 5+1 yalikuwa mapatano muhimu sana katika uga wa kulinda amani na usalama wa kimataifa.

Lakini Marekani ilitangaza mwezi Mei mwaka huu wa 2018 kuwa inajiondoa katika JCPOA, uamuzi ambao ulikosolewa na pande zilizo salia katika mapatano hayo. Baada ya kuondoka Marekani katika JCPOA, kundi la 5+1 lilibadilika na kuwa 4+1 na linasisitiza kuhusu kulindwa mapatano hayo ya nyuklia ili faida zilizokusudiwa zipatikane. Nchi za 4+1 zinasisitiza kuhusu kuchukua hatua za kivitendo ili kuishawishi Iran iendelee kufungamana na JCPOA.

Kuhusiana na hilo wanachama wa 4+1 wanasisitiza kuhusu kufungamana kwao na JCPOA. Ofisi ya Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya, baada ya mkutano wake na Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ilitoa taarifa na kusema: "Pande mbili zina azma ya kulinda JCPOA ambayo ni kati ya nguzo za usalama wa eneo. Umoja wa Ulaya unasisitiza kuhusu kulinda mapatano ya kimataifa."

Taarifa hiyo inaonyesha mueleko jumla wa Umoja wa Ulaya na wanachama wa JCPOA barani Ulaya yaani Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. 

Kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya, kusambaratika na kubatilishwa JCPOA kutakuwa na athari hasi sana kwa amani na usalama wa kimataifa na wakati huo huo kutia dosari kubwa itibari ya kidiplomasia ya Umoja wa Ulaya. Uzingatiaji huo umepelekea viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya akiwemo Mogherini wasisitize kuhusu kulindwa JCPOA na kuhakikisha kuwa mapatano hayo yanatekelezwa. Kwa hivyo pamoja na kuwepo vita vya kisaikolojia vya Marekani, Umoja wa Ulaya umesisitiza azma yake ya kulinda JCPOA.

Kwa mujibu wa Miguel Arias Cañete, Kamishna wa Nishati katika Umoja wa Ulaya : "Kulinda JCPOA kuna maana ya kuheshimu mapatano ya kimataifa na kuna uhusiano na usalama wa kimataifa.

Nchi za Ulaya, kinyume na Marekani ambayo inadai kuwa Iran haitekelezi JCPOA na kwamba eti mapatano hayo hayana maana katika kudhibiti shughuli za nyuklia za Iran, zinaamini kuwa, si tu kuwa Iran imetekeleza ahadi zake zote katika fremu ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA bali pia zinaamini kuwa imechukua hatua za kuzuia kujiri migogoro ya kieneo na kimataifa.

Kwa hakika, mtazamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu JCPOA ni kuwa mapatano hayo ni ya pande kadhaa za kimataifa na yanaweza kuwa mfano wa kuigwa katika utatuzi wa migogoro mingine ya kimataifa.

Ni kwa msingi huu ndio ndio Umoja wa Ulaya unataka kuchukua hatua  za kivitendo kama vile kutekeleza sheria za kuyapa kinga mashirika yanayofanya biashara na Iran. Aidha Umoja wa Ulaya umebuni mfumo mpya maalumu wa kifedha na Iran uliopewa jina la SPV ili kurahisisha mabadilishano ya kibiashara na nishati kati ya mashirika ya Ulaya na Iran.

Pamoja na hayo, licha ya kutekelezwa duru ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kuanzia Novemba 5, lakini mfumo huo wa SPV haujaanza kufanya kazi. Ni kwa sababu hii ndio Iran ikatoa onyo kali kwa nchi za Ulaya. Akiashiria kadhia hiyo, Ali Akbar Salehi amesema: "Subira ya watu wa Iran inaelekea kufika ukingoni na muda ambao nchi za Ulaya zilikuwa zimepewa kutekeleza kivitendo JCPOA unakaribia kufika ukingoni."

Mbali na nchi za Ulaya zilizo katika JCPOA pia kuna nchi za Mashariki ambazo ni China na Russia na zinasisitiza kuhusu udharura wa kutekelezwa kivitendo JCPOA.

Rais Trump wa Marekani

Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia katika mkutano wake  na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliashiria mtazamo wa pamoja wa pande mbili kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA na ulazima wa pande zote kufungamana na mapatano baina yao na Iran.

Kwa mtazamo wa Russia, kunapaswa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa kunatekelezwa nukta ambazo zitaishawishi Iran iendelee kubakia katika JCPOA.

Lavrov amesema pande zilizosalia katika JCPOA lazima zichukue hatua ili kukabiliana na uamuzi wa Marekani wa kujiondoa katika mapatano hayo. Aidha amesema kuchukuliwe hatua za kukabiliana na vitisho vya Marekani dhidi ya nchi ambazo zinataka kuendeleza ushirikiano na Iran.

Kwa msingio huo inaonekana kuna azma ya kimataifa hasa miongoni mwa nchi za 4+1 katika kulinda mapatano ya nyuklia ya Iran na hii ni habari mbaya kwa utawala wa Donald Trump ambao unadai kuwa kwa kutekeleza vikwazo na kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran unataka Tehran isalimu amri na itii matakwa haramu ya Washington.

 

Tags