Qassemi: "Mfumo wa mabadilishano ya fedha baina ya Iran na Ulaya" unafuatiliwa
(last modified Mon, 03 Dec 2018 15:39:00 GMT )
Dec 03, 2018 15:39 UTC
  • Qassemi:

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Mfumo maalumu kwa ajili ya mabadilishano ya fedha kati ya Iran na Ulaya kwa kifupi SPV ungali unaendelea kufuatiliwa; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshabainisha wazi mategemeo iliyonayo katika suala hilo.

Bahram Qassemi ameyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari wa ndani na nje ya nchi na kuongeza kuwa: Kutokana na sababu maalumu, utaratibu wa utekelezaji mpango huo haujakamilika; lakini Tehran inatilia mkazo udharura wa pande zingine katika mpango huo kuchukua hatua zaidi kwa irada na uzito kamili ili mfumo wa mabadilishano ya fedha kati ya pande mbili uanze kutekelezwa.

Kuhusu kuchukua muda mrefu utekelezwaji wa ahadi ilizotoa Ulaya baada ya hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Mchakato wa utekelezaji mabadilishano ya fedha ni suala linalohitajia muda; na ugumu na utata wa suala lenyewe pamoja na mashinikizo laisal kiasi yanayotolewa na Marekani yamekuwa yakikwamisha suala hilo.

Akijibu suali kuhusu wimbi jipya la propaganda za Marekani dhidi ya mpango wa makombora wa Iran na kauli iliyotolewa na Brian Hook, mkuu wa Kundi la Uchukuaji Hatua Dhidi ya Iran katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kwamba upo uwezekano wa kutumia chaguo la nguvu za kijeshi dhidi ya Iran, Qassemi amesema: Suala la chaguo la nguvu za kijeshi dhidi ya Iran limeshapitwa na wakati na haliwezi kutekelezwa. Ameongeza kuwa, kutoa kauli hiyo kumethibitisha uwanagenzi wa Hook, kwa sababu Iran ni nchi yenye nguvu na iliyo tofauti na nchi zingine zilizoandamwa na hujuma za kijeshi za Marekani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza pia kuwa: Wakati Marekani inaziuzia nchi za eneo hili silaha angamizi sambamba na kuchochea migogoro, haiwezi katu kuziusia nchi zingine kuhusu suala la kuimarisha uwezo wao wa kujilinda.../  

Tags