Kuunga mkono Palestina; Sera thabiti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran + Video
Ujumbe wa wabunge wa Palestina ukiongozwa na Mahmoud Al Zahar Mkuu wa Mrengo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, katika bunge, ambaye pia ni mwanachama wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, uko mjini Tehran kwa lengo la kufanya mazungumzo na wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ujumbe huo wa wabunge Wapalestina siku ya Jumapili ulikutana na Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran Ali Shamkhani. Vikao hivyo vilikuwa na mazungumzo muhimu sana katika fremu ya msingi wa sera za kigeni za Iran za kuunga mkono ukombozi wa Palestina. Aidha Siku ya Jumamosi ujumbe huo ulikutana na Spika wa Bunge la Iran Ali Larijani.
Kati ya maudhui zilizojadiliwa ni kuwa, suala muhimu na lenye kipaumbele cha kwanza katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa matazamo wa Iran ni kuunga mkono ukombozi wa Palestina na hasa Quds Tukufu (Jerusalem).
Katika mkutano wake na ujumbe huo, Ali Larijani alisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina. Aidha alisema kuna haja ya kuwafahamisha walimwengu kuwa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ndio sababu ya kuunga mkono malengo matukufu ya Wapalestina. Naye Ali Shamkhani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran alisema: "Hatua yoyote ambayo itapelekea kupotoshwa mkondo wa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni ambao ni tishio kuu kwa ulimwengu wa Kiislamu, itahesabiwa kuwa uhaini kwa Waislamu wote duniani.
Waziri wa Mambo ya Iran Mohammad Javad Zarif naye amebainisha masikitiko yake kuhusu hatua ya kuvunjwa bunge la Palestina na kusema hatua hiyo itatumiwa vibaya na Wazayuni. Zarif amesisitiza udharura wa umoja wa taifa la Palestina katika fremu ya muqawama na mapambano ya ukombozi. Mahmoud Abbas jana alitangaza kuwa Bunge la Palestina litavunjwa katika kipindi cha miezi sita ijayo. Kufuatia uamuzi huo, Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, imetoa taarifa na kuonya kuhusu matokeo hatari ya uamuzi huo na kukumbusha kuwa: "...njia pekee ya kupata uhalali ni kupitia mapambano ya silaha na hivyo hatua yoyote ambayo inakinzana na uhalali huu itashindwa na itakuwa na taathira mbaya miongoni mwa Wapalestina."
Ni jambo la kusikitisha kuwa, sera za kuibua mifarakano katika ulimwengu wa Kiislamu zitapelekea kupungua umuhimu wa kadhia ya Palestina na hivyo kupelekea kukandamziwa haki za Wapalestina wanaodhulumiwa. Sera kama hizo zitadhoofisha mrengo wa wapigania ukombozi wa Palestina. Halikadhalika sera kama hizo za kuibua mifarakano ni sawa na kushirikiana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.
Katika miaka ya hivi karibuni, mkondo wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, au kwa maneno mengine kusahau kadhia ya Palestina unaendelea kwa lengo la kufuatilia machaguo kama vile kurejea katika mipaka ya 1967 au kile kinachotajwa kuwa eti ni muamala mkubwa wa karne.
Sadeq Maliki, mtaalamu na mchambuzi wa kisiasa anaamini kuwa, "Hatua kama vile kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu ni indhari na pia ni uhakika mchungu. Kutekelezwa sera hizi kunaweza kuwa sehemu ya kuangamiza taifa la Palestina."
Mrengo wa mapambano ambao umesimama kidete dhidi ya utawala haramu wa Israel hautaruhusu utawala huo utekeleze njama zake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mkutano wake na ujumbe wa wabunge wa Palestina amesema, licha ya kuwepo baadhi ya tofauti, Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuwa kitu kimoja katika suala la kuiunga mkono Palestina, ili kuepusha utumiwaji mbaya wa suala hilo; na akafafanua kwa kusema: Ni jambo la kusikitisha kuona, leo hii hatua dhidi ya Muqawama zinachukuliwa ndani ya ulimwengu wenyewe wa Kiislamu.
Matukio ya eneo yanaonyesha kuwa, kuna baadhi ya tawala za Kiarabu zinatekeleza njama za kulifanya taifa la Palestina na Quds Tukufu viwe mhango wa sera zao. Hii ni katika hali ambayo muqawama na mapambano ya ukombozi ni jambo linalotambuliwa rasmi katika hati ya Umoja wa Mataifa kama njia ya kisheria ya kukabiliana na ukaliaji mabavu. Sera thabiti za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuunga mkono watu wanaodhulumiwa katika kukabiliana na madhalimu. Hii ndio nukta iliyosisitizwa na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran Ali Skhamkani wakati wa mkutano wake wa wabunge Wapalestina hapa mjini Tehran.