Dakta Zarif: Tangu awali kuweko Marekani nchini Syria kulikuwa kinyume cha sheria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50402-dakta_zarif_tangu_awali_kuweko_marekani_nchini_syria_kulikuwa_kinyume_cha_sheria
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, katu Marekani haijawahi kupambana na kundi la kigaidi la Daesh na kwamba, Washington haikuwa nchini Syria kwa faida ya wananchi wa nchi hiyo wala kwa ridhaa ya serikali ya Damascus.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 25, 2018 02:58 UTC
  • Dakta Zarif: Tangu awali kuweko Marekani nchini Syria kulikuwa kinyume cha sheria

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, katu Marekani haijawahi kupambana na kundi la kigaidi la Daesh na kwamba, Washington haikuwa nchini Syria kwa faida ya wananchi wa nchi hiyo wala kwa ridhaa ya serikali ya Damascus.

Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na Televisheni ya al-Mayadeen na kusisitiza kwamba, tangu awali uwepo wa Marekani nchini Syria haukuwa halali na hakuna taarifa za kutosha kuhusiana na mpango wa Washington huko Syria.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha pia kuwa, tangu Marekani ilipojiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Tehran imekuwa na machaguo kadhaa na kwamba, taifa hili litachagua na kutekeleza moja ya machaguo hayo kulingana na manufaa na maslahi ya kitaifa.

Wanajeshi wa Marekani nchini Syria

Amesema kuwa, madola ya Ulaya yanapaswa kutekeleza majukumu yao na kwamba, endapo hayatapiga hatua kivitendo, Iran haitakaa na kusubiri hilo lifanyike bali itachukua hatua zitakazoendana na maslahi ya nchi.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, madola ya kanda hii ya Mashariki ya Kati hayapaswi kufanyiana uadui bali usalama wa eneo hilo unapaswa kulindwa kwa sura na njia ya pamoja.

Muhammad Javad Zarif ameashiria vita na mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake huko nchini Yemen na kusema kuwa, licha ya utawala wa Aal Saud kutumia makumi ya mabilioni ya dola katika hujuma hiyo lakini umeambulia patupu na haujafikia malengo yake.