Brigedia Jenerali Salami: Iran imeisababishia matatizo mengi kambi ya kibeberu
Katika wakati huu wa kuelekea kwenye Bahman 22, (Februari 11), siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Naibu wa Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran ni kgezo cha utekelezaji wa fikra ya siasa katika Uislamu kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika uhusiano wa kimataifa, kigezo ambacho kimeuletea matatizo makubwa mfumo wa kibeberu.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Brigedia Jenerali Hossein Salami akisema hayo katika kikao cha Jumamosi za Mapinduzi ya Kiislamu kilichopewa jina la "Miaka 40 ya Njama, Miaka 40 ya Muqawama" kilichofanyika hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, kwa kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, ulimwengu wa Kiislamu umeweza kuyaletea mataifa ya dunia maana mpya ya uhusiano wa kimataifa na kwa mara ya kwanza dini hiyo ya Mwenyezi Mungu imetumia vizuri muundo wake wa kisiasa kuunda utawala wa Kiislamu katika zama hizi.
Ameongeza kuwa, ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran ni mpana na umeathiri eneo kubwa la dunia kama ambayo umeyachorea madola ya kibeberu mustakbali hatari sana, na kuzitia hatarini siasa za kiistikbari za madola hayo.
Naibu huyo wa Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH vile vile amesema, Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran yameleta mabadiliko makubwa katika medani na uwanja wa fikra za kimataifa kuhusu nguvu na utawala kama ambavyo yameweza pia kuiunganisha jiografia ya ulimwengu wa Kiislamu na ya wanyonge duniani licha ya kwamba kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa imesambaratika.