Iran yalaani hujuma ya kigaidi nchini Kenya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani hujuma ya kigaidi iliyojiri katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi hiyo jana na kusababisha watu kadhaa kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Katika taarifa yake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi mbali na kulaani hujuma hiyo ya kigaidi pia ametuma salamu za rambi rambi kwa serikali na watu wa Kenya kufuatia kuuawa raia wa nchi hiyo.
Bahram Qasemi amesema Iran iko pamoja katika majonzi na familia za waathirika wa tukio hilo ambalo amesema ni dhidi ya ubinadamu.
Mapema leo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema watu 14 wameuawa katika shambulio la kigaidi lililotokea kwenye hoteli ya kifahari ya DusitD2. Kenyatta pia amesema watu 700 wameokolewa na vyombo vya ulinzi na usalama katika oparesheni iliyoanza jana alasiri na kumalizika mapema leo. Aidha amesema magaidi wote waliohusika katika hujuma hiyo wameangamizwa. Kundi la kigaidi la Al Shabab limedai kuhusika na shambulizi hilo.