Kiongozi Muadhamu: Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum kinapaswa kutatua matatizo
(last modified Sun, 27 Jan 2019 15:49:51 GMT )
Jan 27, 2019 15:49 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum kinapaswa kutatua matatizo

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, kujibu maswali na mahitajio ya kifikra ya vijana, wanafunzi na makundi yenye taathira katika jamii ni kati ya majukumu ya Idara ya Kuutangaza Uislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei ameyasema hayo katika mkutano na wakuu wa Idara ya Kuutangaza Uislamu ya Iran na huku akiwapongeza kwa kazi walizofanya na kusema kuwa kuwepo fikra mpya na ubunifu katika Idara ya Kuutangaza Uislamu ni jambo zuri ameongeza kuwa: "Zama hizi ni zama za mapinduzi, kazi na harakati za kusonga mbele."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria maswali mbalimbali wanayokabiliana nayo wahusika katika sekta za  utamaduni na sanaa na kusema: "Kutoa majibu kuhusu maswali  hayo ni moja ya majukumu ya taasisi kama hii ya Idara ya Kuutangaza Uislamu."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei amesema, Idara ya Kuutangaza Uislamu inapaswa kujikita zaidi katika kazi za Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum na hasa katika kadhia ya kuutangaza Uislamu kwenye Intaneti.

Kiongozi Muadhamu amesema: "Taasisi mbalimbali hivi sasa ziko katika Intaneti lakini uwepo huo unapaswa kuwa ni wa kubuni mada (zenye maana) na kwamba njia bora zaidi ya kutambua na kuwa na uhusiano athirifu na makundi ya kiutamaduni na kupata maswali na fikra zao ni kutumia mitandao ya Intaneti.

Ayatullah Khameneo pia amesema, kuna ulazima wa kuchapishwa vitabu vyenye maudhui za kujibu maswali ya vijana na wanafunzi.