'Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamesimama imara'
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameashiria njama za maadui dhidi ya Iran na kusema: "Pamoja na kuwepo uhasama wote huo, lakini Mapinduzi ya Kiislamu yamesimama imara na yanaendelea kupata nguvu na izza."
Brigedia Jenerali Ramadhan Shariff, msemaji wa IRGC alitoa kauli hiyo Ijumaa katika mji wa Bushehr kusini mwa Iran na sambamba na kutoa salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuanza maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Maadui wanatumia njia kadhaa ili kuonyesha kuwa eti mfumo wa Kiislamu wa Iran haujafanikiwa lakini watu wa Iran wanafahamu vyema propaganda kama hizo zinaenezwa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na maadui sugu wa mfumo wa Kiislamu."
Brigedia Jenerali Shariff ameendelea kusema kuwa, Wamarekani wanaeneza propaganda kuwa nchi ambayo haishirikiani na Marekani haiwezi kustawi lakini kinyume na hilo, "Mapinduzi ya Kiislamu yamekuwa na baraka nyingi na kila uchao yanaendelea kustawi na kupata mafanikio makubwa."
Ikumbukwe kuwa, miaka 40 iliyopita tarehe 12 Bahman mwaka 1957 Hijria Shamsia (Februari 1 1979) Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15.
Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia. Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, yaani Februari 11, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi". Katika siku hizo, kila mwaka hufanyika sherehe kubwa za maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.