'Jeshi la Iran liko imara kuilinda Jamhuri ya Kiislamu'
Luteni Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Iran amesema kuwa, jeshi hilo liko imara katika kuyalinda Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Brigedia Jenerali Kiumars Heidari akisema hayo wakati huu wa kukaribia Siku ya Jeshi nchini Iran.
Ameongeza kuwa, jeshi la Iran halizembea hata sekunde moja kuulinda Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba kusimama kwake huko imara kunathibitishwa na jinsi jeshi hilo lilivyo na fakhari ya kutoa mashahidi 48 elfu katika njia ya haki.
Brigedia Jenerali Kiumars Heidari ameongeza kuwa, jeshi la Iran lina tofauti kubwa na majeshi ya nchi nyingine duniani na kusisitiza kuwa, leo hii jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limekuwa mtetezi mkubwa wa wanyonge na watu wanaodhulumiwa duniani na limesimama imara kukabiliana na waistikbari na mabeberu na ndio maana linapendwa na linakubalika.
Ikumbukwe kuwa kesho Jumapili inayosadifiana na tarehe 17 Aprili ni siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa ratiba tofauti.