Salehi: Ushirikiano wa Iran na Ulaya unaendelea katika miradi ya nyuklia
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran amesema kuwa ushirikiano kati ya Iran na Ulaya katika miradi mbalimbali ya kinyuklia unapiga hatua nzuri.
Ali Akbar Salehi ameongeza kuwa Ulaya imeahidi kutoa yuro milioni 20 kwa ajili ya kujenga kituo bora zaidi cha usalama wa kinyuklia nchini Iran katika Asia Magharibi. Dakta Salehi aliyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari pambizoni mwa ziara yake ya kuyatembelea maonyesho ya kitaifa ya mafanikio ya nyuklia hapa Tehran.
Ali Akbar Salehi aidha alibainisha namna Iran hivi sasa inavyoweza kubuni vinu vya utafiti vya nyuklia na kueleza kuwa iwapo nchi jirani zitaonyesha hamu yao ya kwa vinu hivyo vya utafiti vya maji mazito, zinaweza kushirikiana na Iran.
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran amesisitiza kuwa sekta ya nyuklia ya Iran haijasitishwa na kuongeza kuwa ushirikiano wa Iran na Ulaya katika sekta za kiufundi unapiga hatua vizuri na akasema kuwa hata miradi ya Ulaya inafanyika hapa Iran. Kuhusu mfumo wa fedha wa Ulaya unaojulikana kwa jina la INSTEX, Salehi amesema kuwa nchi za Ulaya zimechukua hatua yenye kuleta matumaini katika uga wa kiuchumi. Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza Alhamisi iliyopita walitangaza mwishoni mwa kikao cha Umoja wa Ulaya kuhusu kusajiliwa mfumo wa mabadilishano ya kifedha baina ya Ulaya na Iran unaojulikana kwa jina la Instrument in Support of Trade Exchanges (INSTEX).