Iraq: Tutaendeleza zaidi uhusiano mwema na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Mshauri wa Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, licha ya vikwazo na mashinikizo ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Baghdad itaendeleza uhusiano wake na Iran ikiwemo sekta ya nishati.
Abdul Karim Hashem Mostafa, ameyasema hayo katika kongamano la Valday nchini Russia ambapo sambamba na kupinga mashinikizo ya Marekani yanayoitaka Iraq kuacha kununua gesi asilia na umeme kutoka Iran, ameongeza kwamba Baghdad imekuwa ikiieleza Washington kwamba haitoshirikiana nayo katika siasa zake ndani ya eneo la Mashariki ya Kati. Kadhalika Mostafa ameashiria safari ya hivi karibu ya Rais wa Benki Kuu ya Iran mjini Baghdad na kusema kuwa, katika safari hiyo nchi mbili zilijadili mapendekezo ya kibiashara kwa kutumia sarafu ya Euro na pia matumizi ya sarafu ya Dinar ya Iraq.
Hivi karibuni Abdolnaser Hemmati, Rais wa Benki Kuu ya Iran akiwa mjini Baghdad alisema kuwa, kwa sasa Iran na Iraq zina mabadilishano mazuri ya kibiashara na kwamba ameamua kufanya safari hiyo kwa ajili ya kuondoa baadhi ya matatizo katika mabadilishano ya kibenki na fedha ya nchi hiyo.
Abdolnaser Hemmati na Ali Al Alaq, Rais wa Benki Kuu ya Iraq walitiliana saini makubaliano ya ulipaji fedha kati ya nchi mbili. Inafaa kuashiria kuwa, ni muda sasa ambapo Marekani imekuwa ikiishawishi serikali ya Iraq kushirikiana na Washington katika kuiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jambo ambalo limekuwa likipingwa vikali na viongozi wa nchi hiyo ya Kiarabu.