Feb 21, 2019 07:01 UTC
  • Iran na China, washirika wa kistratijia barani Asia

Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran (Bunge) na Rais wa China wamesisitiza udharura wa kupanuliwa zaidi ushirikiano wa kistratijia wa nchi hizo mbili.

Dakta Ali Larijani alasiri ya jana alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing. Ameashiria uhusiano wa kihistoria na kirafiki wa nchi hizo mbili na kusema kuwa: China na mshirika wa kistratijia na wa kuaminika wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kwa upande wake, Rais Xi Jinping wa China amelipongeza taifa la serikali ya Iran kwa kuadhimisha miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema, China inataka kupanua zaidi ushirikiano wa kistratijia na Iran.

Iran na China zina uhusiano wa miaka mingi na wa kihistoria na daima zimekuwa zikifanya jitihada za kuimarisha uhusiano huo. Vilevile kudumishwa ushirikiano wa kiuchumi wa China na Iran katika kipindi cha vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ni ishara ya uhusiano wa kistratijia wa nchi hizo mbili ambao umeashiriwa na Rais Jinping katika mazungumzo yake na Spika Larijani.

Larijani na Jinping

Safari ya Larijani na ujumbe wa ngazi za juu wa Iran nchini Uchina na mazungumzo yake na rais wa nchi hiyo vinavyofanyika wakati huu ambapo Marekani inafanya jitihada za kutaka kuitenga Iran kwa kutumia vikwazo vya aina mbalimbali, ni ishara ya umuhimu wa uhusiano baina ya Beijing na Tehran. China daima imekuwa pamoja na Iran katika vipindi mbalimbali vya vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, na ujumbe wa msimamo huo wa China ni kwamba, sera za kutumia mabavu na za kujichukulia mamuzi ya upande mmoja za Washington katika masuala ya kimataifa haziwezi kukubalika. 

Kuhusiana na suala hilo balozi wa zamani wa Iran nchini China, Sayyid Hussein Malaik anasema: China haitambui rasmi vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na ina njia nyingi za kuweza kuendeleza uhusiano wake wa kibiashara na Iran.

Sisitizo la Rais wa China la kuimarishwa zaidi ushirikiano wa nchi hiyo na Iran lina maana ya kujitenga Beijing na siasa haribifu za Marekani dhidi ya Iran. China ambayo inatambulika kuwa nguvu kubwa ya kimataifa na yenye taathira katika masoko ya kiuchumi na kibiashara duniani, daima imekuwa ikipinga sera za serikali ya Washington za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Katika upande mwingine Iran na China zina mitazamo inayofanana kuhusiana na amani ya kimataifa na ushirikiano wa pande kadhaa, na suala hilo limekuwa sababu na kuzidishwa ushirikiano wa Tehran na Beijing katika nyanja mbalimbali.

Katika mazungumzo yake ya Jumanne iliyopita na mwenzake wa China, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Muhammad Javad Zarif aliashiria umuhimu wa uhusiano wa pande hizo mbili na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uhusiano mkubwa zaidi wa kistratijia na Jamhuri ya Watu wa China kuliko nchi yoyote nyingine duniani.  

Muhammad Javad Zarif

Ushirikiano wa Iran na China unahusu nyanja na masuala mengi na mbali na ushirikiano wa pande hizo mbili katika masuala ya kiuchumi na kibiashara ambao umeifanya Beijing kuwa mshirika wa kuaminika wa Tehran, nchi hizo mbili pia zinashirikiana katika masuala mengi ya kimataifa.

Uungaji mkono wa China kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA kwa kifupi ikiwa pamoja na Russia vinaonesha kuwa, sera za Jamhuri ya Kiislamu za kujielekeza mashariki mwa dunia badala ya Magharibi ni sahihi na za kimantiki.  

Tags