Zarif: Ulaya haina uwezo wa kufanya lolote mbele ya Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Nchi za Ulaya hazina uwezo wa kufanya lolote mbele ya Marekani.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mazungumzo maalumu ya kubainisha mwenendo wa nchi za Ulaya kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na mpango wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran juu ya suala hilo. Zarif amefafanua kuwa: Tangu awali nchi za Ulaya zilikuwa zikiyatazama makubaliano ya JCPOA kama suala la matunda na mafanikio, lakini ukweli ni kwamba hazina na uwezo wa kutosha wa kusimama imara kukabiliana na vikwazo vya Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa: Nchi za Ulaya zimefanya jitihada kadhaa kuhusu JCPOA, lakini kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, jitihada hizo hazikuwa za kutosha na hata katika baadhi ya masuala jitihada hizo zilidhihirisha jinsi nchi za Ulaya zilivyokuwa haziko tayari kugharimika.
Dakta Zarif amesema, Iran imejaribu kuzifanya nchi za Ulaya zitekeleze wajibu na ahadi zao zilizotoa katika JCPOA na akafafanua kwamba: Kuhusiana na suala hilo na katika upande wa kidiplomasia, Iran imeendelea kufanya kazi na nchi za Ulaya lakini katu haijaielekeza matumaini yake yote kwa nchi hizo.
Kuhusiana na kipaumbele cha sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Zarif amesema: Viongozi wa Iran wamekuwa na mawasiliano zaidi na nchi jirani na washirika wake wa jadi kama Russia, China na Uturuki.
Katika hotuba ya Nouruzi aliyotoa katika Haram ya Imam Ridha (as) huko mjini Mashhad, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei alisema: Katika kadhia ya JCPOA, jukumu la nchi za Ulaya lilikuwa ni kusimama imara kukabiliana na Marekani, lakini hazikufanya hivyo kwa visingizio mbali mbali na kiuhalisia hasa ni kwamba zimejitoa kwenye JCPOA; kwani hata zimeiwekea Iran vikwazo vingine vipya.../