Mazungumzo ya Rais Rouhani na Waziri wa Mambo ya Nje wa India
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kuimarishwa uhusiano kati ya Iran na India ni kwa maslahi ya usalama na ustawi wa kiuchumi wa eneo.
Rais Hassan Rouhani jana alikutana kufanya mazungumzo hapa Tehran na Bi Sushma Swaraj Waziri wa Mambo ya Nje wa India. Katika mazungumzo hayo Rais Rouhani ameashiria uwezo na suhula zilizonazo nchi mbili hizi na kuongeza kuwa Tehran na New-Delhi zina malashi mengi ya pamoja na vile vile akasema, nchi hizi zinaweza kuwa na ushirikiano mkubwa kwa kustawisha kistratejia uhusiano wao wa kiuchumi katika uga wa kisiasa na katika masuala ya kieneo na kimataifa.
Rais wa Iran amezitaja safari za hivi karibuni na zijazo za viongozi wa ngazi za juu wa Iran na India katika nchi mbili hizi kwa ajili ya kuboresha uhusiano na kueleza kuwa, uchumi wa Iran na India unategemeana na kwamba Iran ina uwezo wa kuwa msingi wa kutumainiwa katika kudhamini nishati inayojitajika kiuchumi.
kwa upande wake Sushma Swaran Waziri wa Mambo ya Nje wa India amesema kuwa nchi yake inataka kustawisha uhusiano na Iran katika nyanja zote. Swaraj amesema kuwa muungano imara wa mataifa mawili ya Iran na India ni sababu inayopelekea kuimarishwa ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya serikali hizi mbili na kuongeza kuwa India ikiwa ni nchi yenye uchumi unaokuwa kwa kasi na inayohitajia nishati, inataka kuwa na msingi wa uhusiano wa pamoja kwa maslahi ya nchi mbili na kwamba uhusiano huo unapasa kuwa zaidi ya ushirikiano wa kibiashara.
Waziri wa Mambo ya Nje wa India pia amefanya mazungumzo na mwenzake wa Iran Muhammad Javad Zarif ambapo wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni na kuimarishwa uhusiano wa pande mbili, kieneo na kimataifa.