Apr 28, 2019 07:10 UTC
  • Kongamano la Mustakabali wa Ulimwengu wa Kiislamu laanza Tehran

Kongamano la Mustakabali wa Ulimwengu wa Kiislamu katika Dira ya Mwaka 2035 limeng'oa nanga hii leo hapa katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran, kwa kuwaleta pamoja wanazuoni na wajumbe kutoka nchi mbalimbali duniani.

Kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran limefunguliwa rasmi na Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Dakta Ali Larijani.

Wanazuoni na wanafikra kutoka Iran na nchi nyingine kama vile Uturuki, Iraq, Misri, Tunisia, Lebanon, Algeria, Ufaransa, Finland, Austria na Australia wanashiriki mkutano huo.

Aidha mabalozi wa nchi kadhaa za Kiislamu wanahudhuria mkutano huo, mbali na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Iran na makamanda wa kijeshi.  

Spika wa Bunge la Iran, Dakta Ali Larijani

Wanaakademia, watafiti na wanafikra kutoka Chuo Kikuu cha Tehran wanaoshiriki mkutano huo, wanatazamiwa kuwasilisha mada mbalimbali katika kikao hicho cha kimataifa kitakachomalizika kesho Jumatatu.

Miongoni mwa maudhui zinazotamiwa kujadiliwa katika kongamano hilo ni mustakabali wa sera za usalama wa ulimwengu wa Kiislamu, maendeleo ya kiuchumi, ustaarabu, utamaduni na thamani za ulimwengu wa Kiislamu, pamoja na mustakabali wa masuala ya mazingira, sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa Kiislamu. 

Tags