Jeshi la Majini la Iran: Maadui hawawezi kuthubutu kuishambulia Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53482-jeshi_la_majini_la_iran_maadui_hawawezi_kuthubutu_kuishambulia_iran
Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maadui hawana ubavu wala uthubutu wa kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu kutokana na uwezo mkubwa wa kijeshi na kiulinzi wa taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 14, 2019 07:16 UTC
  • Jeshi la Majini la Iran: Maadui hawawezi kuthubutu kuishambulia Iran

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema maadui hawana ubavu wala uthubutu wa kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu kutokana na uwezo mkubwa wa kijeshi na kiulinzi wa taifa hili.

Admeri Hussein Khanzadi amepuuzilia mbali uwepo wa manowari na meli za kijeshi za Marekani katika Ghuba ya Uajemi na kubainisha kuwa, "Sijui kwa nini habari ya kuwepo meli hizo inachangamkiwa kiasi hiki. Madhali vikosi vya majini vya Jamhuri ya Kiislamu vinalinda mipaka yake, adui hawezi kujaribu kuliletea chokochoko taifa la Iran."

Ameeleza bayana kuwa, uwepo wa vikosi vya Marekani katika Ghuba ya Uajemi ni wa kimaonyesho tu na usio na maana, na kwamba vinapaswa kuondoka katika eneo hili haraka iwezekanavyo.

Admeri Khanzadi amebainisha kuwa, vikosi vya Marekani vimekuwa karibu na mipaka ya Iran katika kipindi chote cha miaka 40 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini uwepo huo haujawa na maana yoyote na kusisitiza kuwa, vikosi vya Iran vitaendelea kulinda mipaka yake kwa nguvu zote. 

Boti za kivita za Iran katika Ghuba ya Uajemi

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kuwa jeshi la majini la Iran lipo tayari kukabiliana na vitisho vya maadui na kuongeza kuwa Iran inapiga hatua haraka katika kujitegemea kwa lengo la kudhamini amani na maslahi yake.

Haya yanajiri huku ripoti zikidokeza kuwa, Marekani inajiandaa kutuma wanajeshi 120,000 katika eneo la Asia Magharibi eti kwa ajili ya 'kuikabili Iran'.