Kwa mara nyingine EU yapinga siasa za Marekani kuhusu Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani kwa mara nyingine amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya unapinga siasa za Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa siasa hizo za kiuadui hazisaidii chochote.
Heiko Maas alisema hayo jana (Jumamosi) katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Passauer Neuen Presse la nchini Ujerumaini na kuongeza kuwa, kitendo cha Marekani cha kujitoa kivyake-vyake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA hakikuwa sahihi hata kidogo na kwamba Umoja wa Ulaya una imani na mazungumzo na sio malumbano na kushadidisha vita vya maneno.
Naye Omid Nouri Pour, msemaji wa Chama cha Kijani cha Ujerumani sambamba na kuunga mkono msimamo wa Umoja wa Ulaya wa kupinga siasa za kibeberu za Marekani kuhusu Iran, amelalamikia kucheleweshwa utekelezaji wa njia mbadala ya mabadilishano ya kifedha baina ya Iran na Umoja wa Ulaya maarufu kwa jina la INSTEX uliobuniwa baada ya Marekani kutishia kuyawekea vikwazo mashirika yatakayoshirikiana kibiashara na Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani alisema baada ya Marekani kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA tarehe 8 Mei 2018 kwamba nchi za Ulaya zimeanzisha mfumo wa Swift wa mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi za Ulaya na Iran.
Baada ya Marekani kurejesha vikwazo vya kidhulma dhidi ya Iran, nchi za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ziliiahidi kudhamini manufaa ya kiuchumi ya Iran ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na na kuisihi Tehran isijitoe.
Hata hivyo na licha ya nchi hizo kupinga kimaneno siasa za kibeberu za Marekani, lakini hadi hivi sasa zimeshindwa kutekeleza kivitendo ahadi zao kwa Iran.