Iran inatazamia kusherehekea siku kuu ya Idul Fitr Jumatano ya Juni 5
Wananchi Waislamu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanatazamiwa kusherehekea siku kuu ya Idul Fitr siku ya Jumatano, Juni 5.
Hayo yametangazwa na Alireza Movahednejad, mwanachama wa timu ya kufuatilia kuandama kwa mwezi wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Amesema timu ya wataalamu elfu moja kutoka ofisi hiyo itatumwa kufuatilia mkondo wa mwezi kesho jioni katika maeneo mbalimbali ya Iran.
Amesema matokeo ya uchunguzi wao yatatumwa kwa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na iwapo itathibiti basi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, atathibitisha na kuitangaza Jumatanbo ya Juni 5 kuwa tarehe Mosi Shawwal 1440 Hijria Qamaria, ambapo Waislamu wa hapa nchini wanatazamiwa kuungana na wenzao duniani katika sherehe za Idul Fitr.
Wataalamu hao wa mwezi hapa nchini watafuatilia kuthibitisha iwapo kesho Jumanne itakuwa siku ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani au la.
Taarifa ya ofisi hiyo imeongeza kuwa, iwapo itathibiti, Sala ya Idul Fitr itaongozwa na Ayatullah Ali Khamenei mwendo wa saa mbili asubuhi kwa saa za hapa nchini katika Uwanja wa Sala wa Imam Khomeini MA hapa mjini Tehran Jumatano.
Sherehe za Idi zinatanguliwa na Sala ya Idul Fitri kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukamilisha ibada adhimu ya funga ambayo ni nguzo muhimu katika dini ya Kiislamu.