Jun 12, 2019 04:27 UTC
  • Iran inaongoza katika vita dhidi ya mihadarati duniani

Katibu Mkuu wa Idara ya Kupambana na Mihadarati nchini Iran amezikosoa nchi za Ulaya kwa sababu ya kutolipa uzito suala ya kupambana na mihadarati. Aidha amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaongoza katika kupambana na mihadarati duniani."

Brigedia Jenerali Eskandar Momeni, Katibu wa Idara ya Kupambana na Mihadarati Iran ameyasema hayo Jumanne katika kikao cha waandishi habari ambapo amefafanua kuhusu hatua ambazo Iran imechukua katika kukabiliana na mihadarati au dawa za kulevya na kusema: "Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kunasa asilimia 75 ya afiuni, asilimia 61 ya morphine na asilimia 17 ya heroini yote iliyonaswa duniani."

Aidha amesema: "Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, katika mwaka 2017, Iran iliweza kunasa tani 21 za heroini katika hali ambayo bara Ulaya lenye jumla ya nchi zaidi ya 50 zimenasa jumla ya tani nne tu za heroini katika kipindi hicho."

Askari wa Marekani wakiwa katika mashamba ya afiuni nchini Afghanistan

Katibu Mkuu wa Idara ya Kupambana na Mihadarati Iran ameendelea kusema kuwa, nchi ambazo zinalengwa na wafanya biashara haramu ya dawa za kulevya hazipaswi kupuuza mapambano ya mihadarati. Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, Iran imefanikiwa kunasa tani 12 elfu za aina mbali mbali ya mihadarati na pia maafisa usalama 3,814 Wairani wameuawa shahidi katika vita dhidi ya mihadarati huku wengine 12,000 wakijeruhiwa.

Brigedia Jenerali Momeini ameendelea kusema kuwa, tokea Marekani iivamie kijeshi Afghanistan, uzalishaji wa dawa za kulevya nchini humo umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Amesema katika mwaka 2000 na 2001, ukulima wa mihadarati Afghanistan ulikuwa ni tanu 200 lakini baada ya askari wa Marekani kuvamia nchi hiyo, kiwango hicho kimeongezeka na kufika takribani tani 10,000.

Katibu Mkuu wa Idara ya Kupambana na Mihadarati nchini Iran amesema karibu Wamarekani milioni 20 walioa na umri wa zaidi ya miaka 12 wanatumia dawa za kulevya na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Marekani, katika mwaka 2017,  Wamarekani 70,237 walipoteza maisha kutokana na na utumizi wa mihadarati.

 

Tags