Iran yaitaka Marekani iangamize silaha zake za kemikali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54420-iran_yaitaka_marekani_iangamize_silaha_zake_za_kemikali
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitakidi kuwa, dunia itakuwa pahala salama iwapo Marekani itaangamiza silaha zake hatari za kemikali.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 28, 2019 10:34 UTC
  • Iran yaitaka Marekani iangamize silaha zake za kemikali

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitakidi kuwa, dunia itakuwa pahala salama iwapo Marekani itaangamiza silaha zake hatari za kemikali.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo Ijumaa kwa mnasaba wa kukumbuka mashambulizi ya mabomu ya kemikali yaliyofanywa na utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya wananchi wa Iran miaka 32 iliyopita.

Zarif ameongeza kuwa Iran ni mwanachama hai wa Shirika la Upigaji Marufuku Silaha za Kemikali (OPCW) na imekuwa ikifanya jitihada za kujaribu kuangamiza kikamilifu silaha zote za sumu duniani.  Amesema Iran ni moja ya waathirika wakuu wa silaha za kemikali.

Amesema Marekani ambayo ndiye mmiliki pekee wa silaha za kemikali duniani, inapaswa kuharibu kikamilifu silaha zake za maangimivu ili dunia iwe pahapa salama bila silaha hizo hatari za kemikali.

Wananchi wa Iran wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi kwa mnasaba wa kuwaenzi na kuwakumbuka makumi ya wananchi wa Iran waliouawa shahidi katika mashambulizi hayo ya silaha za kemikali, katika mji wa Sardasht magharibi mwa Iran. 

Baadhi ya wahanga wa mashambulizi ya Sardasht

Raia wasio na ulinzi karibu 150 wa Iran wakazi wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya utawala wa zamani wa Saddam Hussein wakati wa vita vya Iraq dhidi ya Iran mnamo Juni 28 na 29 mwaka 1987.

Wakati huohuo, Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema licha ya kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mhanga mkubwa wa matumizi ya silaha za kemikali, lakini imeendelea kuwa mshirika mkubwa na mwanachama hai katika kampeni na jitihada za kutaka kutokomezwa silaha hizo za maangamivu duniani, zinazofanywa na taasisi ya OPWC.