Rais Rouhani: Kama Marekani inaogopa moto basi haipaswi kuwasha muale
(last modified Wed, 03 Jul 2019 13:01:05 GMT )
Jul 03, 2019 13:01 UTC
  • Rais Rouhani: Kama Marekani inaogopa moto basi haipaswi kuwasha muale

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yana manufaa kwa mataifa yote, eneo la Mashariki ya Kati na dunia nzima na kuongeza kuwa, Kama Marekani inaogopa moto haipaswi kuwasha muale na itekeleze maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika kikao cha baraza la mawaziri hapa mjin Tehran. Ameashiria matamshi yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani kwamba Iran inacheza na moto na kusema: Wamarekani walianza kucheza na moto tangu mwaka mmoja uliopita katika eneo hili na katika hali hiyo ya kuendelea kucheza na moto wanasema: Ni hatari kucheza na moto.

Dakta Rouhani amesema pande zinazoshirikiana na Iran katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA daima zimekuwa zikiiasa Iran ibakie katika makubaliano hayo na kuongeza kuwa: Kama pande hizo hazitatekeleza wajibu na ahadi zao ndani ya makubaliano hayo, Jamhuri ya Kiislamu itachukua hatua inayofuata baada ya siku 60 kama ilivyotangaza hapo kabla.

Ameashiria kuwa Iran imevuka kiwango ya kilo 300 za akiba ya urani iliyorutubishwa kilichoainishwa katika makubaliano ya JCPOA na kusema: Iwapo pande nyingine za makubaliano hayo zitatekeleza majukumu yao, Iran nayo itarejea katika kiwango kilichoainishwa. 

Rais Rouhani katika kikao cha baraza la mawaziri

Rais Hassan Rouhani amekosoa mienendo ya kindumakuwili ya Marekani na nchi za Ulaya kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema kuwa, kama JCPOA ni makubaliano mazuri basi kwa nini Marekani na nchi za Ulaya hazitekelezi majukumu yao ndani ya makubaliano hayo, na kama ni mabaya basi ni kwa nini pale Iran inapoacha kutekeleza baadhi ya vipengele vyake kunapigwa makele mengi duniani? 

Vilevile ameutaja mfumo wa mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na nchi za Ulaya INSTEX kuwa hadi sasa umekuwa hatua ya kimaonyesho tu. Amesema kuwa, mafisa wa Ulaya hawakutekeleza hata yale waliyoiahidi Iran kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amekumbushia tukio la shambulizi la meli ya kivita ya Marekani ya USS Vincennes dhidi ya ndege ya abiria ya Iran tarehe 3 Juni mwaka 1988 na kusema shambulizi hilo dhidi ya ndege ya abiria ya Iran limeonesha kwamba ni rahisi sana kwa Wamarekani kutenda jinai.             

Tags