Waziri wa Ulinzi wa Iran: Hatutaruhusu uharamia wa Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54624-waziri_wa_ulinzi_wa_iran_hatutaruhusu_uharamia_wa_uingereza
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya askari wa Jeshi la Wanamaji la Uingereza ya kuisimamisha meli ya mafuta ya Iran katika Lango Bahari la Jabal al Tariq (Gibraltar) na kueleza bayana kuwa, Tehran kamwe haitaruhusu uharamia huo wa London.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2019 02:15 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Iran: Hatutaruhusu uharamia wa Uingereza

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya askari wa Jeshi la Wanamaji la Uingereza ya kuisimamisha meli ya mafuta ya Iran katika Lango Bahari la Jabal al Tariq (Gibraltar) na kueleza bayana kuwa, Tehran kamwe haitaruhusu uharamia huo wa London.

Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema hayo katika mji wa bandari wa Bandar Abbas ulioko kusini mwa nchi na kufafanua kuwa, "Hatua ya Uingereza ya kusimamisha na kuzuia meli ya mafuta ya Iran ni ukiukaji wa kanuni na sheria za kimataifa, sambamba na kuvunja ahadi za nchini za Umoja wa Ulaya za kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Iran kamwe haiwezi kuvumilia na kuruhusu vitendo hivyo vya uharamia."

Amekumbusha kuhusu hatua ya hivi karibuni ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ya kutungua ndege ya kijasusi ya Marekani ya Global Hawk iliyoingia kinyume cha sheria katika anga ya nchi hii na kusisitiza kuwa, kitendo hicho kilikuwa na ujumbe wa wazi kwamba taifa hili halitamruhusu yeyote akiuke mipaka yake ya angani, ardhini na baharini.

Katika kuhalalisha hatua yake hiyo ya Alkhamisi iliyopita, Uingereza ilidai kwamba inaiuzuilia meli hiyo ya mafuta ya Iran kwa kuwa imekiuka vikwazo vya Marekani na vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria vilivyowekwa mwaka 2011. London ilidai kuwa meli hiyo ya mafuta ilikuwa inaelekea Syria.

Meli ya mafuta ya Iran inayozuiliwa na Uingereza

Hivi karibuni balozi wa Uingereza mjini Tehran aliitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kukabidhiwa malalamiko ya Tehran kuhusu chokochoko hizo za askari wa Uingereza katika Lango Bahari la Jabal al Tariq.

Taarifa ya wizara hiyo ilisema kitendo cha kuizuia meli hiyo ya mafuta ya Iran isiendelee na safari yake ni kinyume cha sheria na ni jaribio la kuzusha mzozo.