Zarif aionya Marekani 'isiichezee Iran'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali uwepo kijeshi wa Marekani katika kila pembe ya dunia na kusema kuwa, kuwepo huko kwa Washington ndio sababu ya "kukosekana amani na uthabiti".
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo mapema leo mara baada ya kuwasili Caracas, mji mkuu wa Venezuela kwa madhumuni ya kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM). Baada ya Venezuela, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran atazitembelea pia Nicaragua na Bolivia.
Dakta Zarif ameeleza kuwa, Marekani inavuruga amani na uthabiti popote pale inapotia mguu wake, na kwamba leo hii uwepo kijeshi wa Washington unavuruga amani na usalama Ghuba ya Uajemi, Mashariki ya Kati pamoja na Amerika ya Latini. Ameongeza kuwa, popote walipokwenda wanajeshi wa Marekani wamepelekea kuongezeka mashinikizo kwa watu wa eneo hilo na kuchochea ugaidi na misimamo ya kufurutu ada.
Akizungumza mapema wiki hii na gazeti la American New Yorker, huko New York makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Dakta Zarif aliashiria chokochoko za hivi karibuni zilizoanzishwa na Marekani katika Ghuba ya Uajemi na kuionya Washington "isiichezee Iran".
"Tunasema, 'mnaweza kuanzisha vita, lakini si nyinyi mtakaovihitimisha," alisema Dakta Zarif na kuongeza kwamba, taifa la Iran litaendelea kuwepo na kustawi kwa miaka na miaka wakati rais wa Marekani Donald Trump akiwa hayupo tena.../