Larijani: Zarif ni nembo ya uchapakazi na diplomasia makini ya Iran
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amemtaja Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni nembo ya uchapakazi na diplomasia makini ya Iran.
Ali Larijani aliyasema hayo jana Jumatatu alipotembelea Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kuzungumza na Waziri Muhammad Javad Zarif. Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amemshukuru Dakta Zarif kwa uchapakazi wake na kueleza kuwa: Katika upande wa diplomasia, Muhammad Javad Zarif amefanya kazi kwa jitihada kubwa na ameleta mafanikio na matunda makubwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amemtaja Waziri wa Mambo ya Nje Dakta Zarif kuwa ni mwanadiplomasia msomi na mwenye tajiriba na kuongeza kuwa, Zarif anatetea maslahi ya Iran kwa umakini mkubwa, kwa busara na bila kuchoka. Amesema: Jitihada zake athirifu zimewafanya maadui wa taifa la Iran wamuwekee vikwazo.
Kwa upande wake Muhamamd Javad Zarif amemshukuru Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran kwa kumtembelea katika Wizara ya Mambo ya Nje na kusema kuwa: Anaunga mkono na kutetea kwa nguvu zote maslahi ya taifa na haki ya Iran katika uga wa kimataifa.
Akizungumza na vyombo vya habari jana mjini Tehran, Ali Rabii Msemaji wa Serikali ya Iran alisema kuwa Zarif ni sawa na chombo cha bahari na kwamba hakuna wakati ambao White House imejipanga na kufanya kila iwezalo dhidi ya Iran kama hivi sasa.
Itakumbukwa kuwa, Wizara ya Fedha ya Marekani Alhamisi iliyopita ililiweka jina la Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hii katika orodha ya shakhsia iliyowawekea vikwazo ikiwa ni katika muendelezo wa uraibu wa serikali ya Marekani kwa maradhi ya vikwazo.