Zarif: Sera za kutumia mabavu zinatoweka duniani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, sera za kuwafuta wengine, kukwepa sheria, kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kufadhilisha maslahi ya kundi moja dhidi ya malahi ya wengine na kuwa tegemezi zimo katika hali ya kutoweka na kuyoyoma.
Muhammad Javad Zarif amesema leo katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na Utukufu wa Mwandamu mjini Tehran kwamba Jamhuri ya Kiislamu haizitambui haki za binadamu kuwa ni wadhifa wa kidini pekee bali pia ni jambo la dharura kwa usalama wake wa kitaifa kwa sababu usalama wake unafungamana na wananchi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa usalama wa taifa wa nchi mbalimbali hauwezi kununuliwa kwa pesa na kuongeza kuwa: Baadhi ya nchi zinaufungamanisha mustakbali na usalama wao na suala la kuwa tegemezi kwa nchi nyingine na kwamba zinaweza kulinda usalama wao kwa kutoa fedha na kununua silaha; hata hivyo nchi hizo hazijajifunga na kupata ibra ya historia.
Zarif amesema kuwa baadhi ya nchi za kanda hii ya Mashariki ya Kati bado zina matumaini kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakalia kwa mabavu ardhi na makazi ya ndugu zao wa Palestina kwa kipindi cha miaka 70 sasa na ambao mfumo wake wa kujikinga na makombora wa Iron Dome hauwezi hata kukabiliana na makombora ya Hamas, unaweza kuwalinda.
Vilevile ameashiria kumbukumbu ya mashambuliizi ya bomu la nyuklia la Marekani huko Hiroshima nchini Japan na kusema: Utawala unaoamini kwamba unaweza kuhitimisha vita kwa kuua mamia ya maelfu ya wanadamu, wanawake, watoto na wanaume, hauwezi kuwa ila na sera za kufuta pande nyingine, kuvamia nchi na kukwepa sheria na kanuni.