Shamkhani: Mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran yamefeli
Taifa la Iran linafahamu kuwa utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani umefeli katika 'mashinikizo ya juu zaidi' dhidi ya Iran.
Hayo yamesemwa na Admeli Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran katika mahojiano na Televisheni ya ABC mjini Tehran na ameongeza kuwa: "Tembea katika mitaa ya Tehran na utaona namna watu wetu walivyo motisha na utafahamu kuwa Marekani haijafanikiwa katika malengo yake."
Halikadhalika Shamkhani ametupilia mbali ile dhana kuwa Rais Trump anataka kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kuwa, kampeni ya vikwazo hailengi kuifanya Iran ikae katika meza ya mazungumzo, bali lengo lake ni kutaka nchi hii isalimu amri. Shamkhani amesisitiza kuwa, maadamu Marekani inatumia mbinu hii, Iran haitafanya mazungumzo na taifa hilo.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran pia amesema Marekani haiwezi kutegemewa kutekeleza mapatano yoyote na Iran katika siku za usoni kwani Trump alichukua hatua ya ghafla ya kuindoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) ambayo yalikuwa yanaungwa mkono na utawala uliopita wa Marekani.

Shamkhani pia amelaani vikali sera za serikkali ya Marekani za kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel katika makabiliano na Wapalestina.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, hatua ya Marekani kuitambua Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Israel ni jambo ambalo limeibua taharuki zaidi katika eneo.