Dakta Zarif: Madola ya Ulaya yatekeleze kivitendo ahadi zao za JCPOA
Waziri wa Mashauri yay Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, endapo madola ya Ulaya yatatekeleza kivitendo ahadi zao za makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, basi Iran nayo iko tayari kuachana na hatua ilizochukua za kupunguza uwajibikaji wake kwa mujibu wa makubaliano hayo.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya France 24 ambapo sambamba na kukaribisha kwa mikono miwili mapendekezo ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesisitiza kwamba, mapendekezo ya Rais wa Ufaransa kwa ajili ya kupunguza mivutano kuhusiana na makubaliano ya nyuklia yapo katika njia nzuri lakini kuna haja ya kufanyika kazi ya ziada.
Akizungumza pasi na kuashiria mapendekezo ya Ufaransa yalikuwa yepi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya unapaswa kutekeleza ahadi ulizotoa kuhusu mapatano ya JCPOA kufuatia hatua ya upande mmoja ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa.
Dakta Zarif aliwasili Paris Alhamisi baada ya kumaliza safari yake mjini Oslo nchini Norway na kabla ya hapo alikuwa amezitembelea Sweden na Finland.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua za kupunguza utekelezaji wa majukumu yake katika JCPOA baada ya pande zingine katika mapatano hayo kutotekeleza ahadi zao. Tehran imesema iwapo pande zingine katika JCPOA zitatekeleza ahadi zao, basi nayo pia itarejea haraka katika utekelezaji wa ahadi zake kikamilifu.
Moja ya ahadi ambazo nchi za Ulaya zilikuwa zimesema zitatekeleza baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA kinyume cha sheria, ni kuanzisha mfumo wa mabadilishano ya kifedha maarufu kama INSTEX lakini bado madola ya Ulaya hayajatekeleza ahadi hiyo.