Baqeri: Utawala wa Kizayuni unazidi kudhoofika
Mkuu wa Kamandi ya Vikosi Vyote vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Kambi ya muqawama (mapambano ya Kiislamu) inazidi kusonga mbele katika kuudhoofisha utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo."
Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Kamandi ya Vikosi Vyote vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo Jumatano mjini Tehran ambapo ameashiria ushindi wa wapiganaji wa mhimili wa muqawama huko Syria, Iraq na Yemen na kusema: "Leo Wayemen wamefika katika hatua ambayo wanajitegemea katika sekta ya kujihami na wana uwezo wa kutungua ndege zisizo na rubani (drone) za kisasa zaidi duniani."
Meja Jenerali Baqeri ameendelea kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya nchi zenye usalama zaidi duniani na kuongeza kuwa: "Maadui hawana uwezo wa kuhujumu na kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran na hilo linatokana na jitihada za kijihadi za usiku na mchana za watu wa Iran."
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ameashiria kutunguliwa drone ya kijasusi ya Marekani ambayo ilikuwa imeingia kinyume cha sheria katika mipaka ya angani ya Iran na kusema Jeshi la Marekani lilitathimini uwezo wa kijeshi na ushawishi wa Iran katika eneo na likafikia natija kuwa haliwezi kujibu pigo hilo la Iran.
Itakumbukwa kuwa tarehe 20 mwezi Juni mwaka huu ndege ya ujasusi ya RQ-4 Global Hawk ya Marekani na baada ya kukiuka anga ya Iran karibu na Kouh-e-Mobarak katika eneo la Jask mkoani Hormozgan kusini mwa Iran, ilitunguliwa na kikosi cha anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).