Dakta Zarif: Iran na Indonesia zina mtazamo mmoja kuhusu kadhia ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55845-dakta_zarif_iran_na_indonesia_zina_mtazamo_mmoja_kuhusu_kadhia_ya_palestina
Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran na Indonesia zina mtazamo mmoja kuhusiana na kadhia ya Palestina na kubainisha kwamba, Baytul-Muqaddas ni kibla cha kwanza cha Waislamu.
(last modified 2025-10-22T06:10:45+00:00 )
Sep 07, 2019 02:38 UTC
  • Dakta Zarif: Iran na Indonesia zina mtazamo mmoja kuhusu kadhia ya Palestina

Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran na Indonesia zina mtazamo mmoja kuhusiana na kadhia ya Palestina na kubainisha kwamba, Baytul-Muqaddas ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Dakta Zarif amesema hayo huko Jakarta mji mkuu wa Indonesia katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenyeji wake Bi Retno Marsudi na kusisitiza kwamba, nchi mbili hizi zinafuatilia malengo ya pamoja kuhusiana na kadhia ya Palestina.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria matukio ya eneo la Asia Magharibi na kusema bayana kwamba, usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi unaweza kupatikana kwa kuweko ushirikiano baina ya nchi za ukanda huu.

Kwa upande wake Bi Retno Marsudi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Indonesia amesisitiza juu ya kupatiwa ufumbuzi hitilafu na mivutano katika eneo la Asia Magharibi kupitia njia ya mazungumzo na akaeleza kwamba, amani ya dunia haiwezi kupatikana pasi na kuweko amani na usalama katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Bendera ya Palestina

Aidha kuhusiana na kadhia ya Palestina, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Indonesia amesema kuwa, nchi yake  inataka kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul-Muqaddas.

Vilevile Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Indonesia amesema kuwa, ni jambo la dharura kwa nchi zote shiriki zilizobakia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kutekelezwa kikamilifu makubaliano hayo.