Oct 18, 2019 16:50 UTC
  • Mamilioni wakusanyika Karbala katika Arubaini ya Imam Hussein (as)

Mamilioni ya Waislamu wanakusanyika katika mji mtakatifu wa Karbaka nchini Iraq kwa ajili ya kushiriki katika shughuli ya Arubaini ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as).

Baadhi ya Waislamu hao wanaokadiriwa kufikia milioni 20 kutoka maeneo mbalimbali ya dunia wameelekea Karbala kwa miguu baada ya kukata masafa ya karibu kilomita 80 kutoka katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq. Wengi kati ya Waislamu hao waliwasili katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala wiki moja kabla, wakijitayarisha kwa ajili ya marasimu na shughuli ya Arubaini ya Imam Hussein inayomaanisha siku ya Arubaini baada ya kuuawa shahidi mjukuu huyo wa Mtume wa Muhammad (saw) ambayo inasadifiana na kesho tarehe 20 Safar.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Abdolreza Rahmani Fazli amesema kuwa, Wairani milioni 3.5 wameingia Iraq kwa ajili ya kushiriki katika shughuli ya Arubaini ya Imam Hussein (as). Amesema idadi hiyo imepita ile ya Wairan walioshiriki kwenye Arubaini ya Imam kwa watu milioni 1.2.

Mamilioni ya Waislamu kutoka nchi nyingine za kigeni pia wamewasili Karbala kwa ajili ya kushiriki katika shughuli hiyo hususan kutoka nchi za Pakistan, Afghanistan, Azerbaijan, Uturuki, india, Kuwait, Bahrain na Lebanon. 

Karbala

Waislamu hao wanakaribishwa na wenzao wa Iraq ambao wanawahudumia kwa kuwapa makazi, chakula, usafiri na huduma nyingine muhimu.

Mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) aliuawa shahidi mwaka 61 Hijria katika ardhi ya Karbala nchini Iraq akiwa pamoja na familia na masahaba zake 72 wakipambana dhidi ya dhulma na upotoshaji uliokuwa ukifanywa na mtawala wa wakati huo Yazid bin Muawiya katika mafundisho ya dini ya Uislamu.

Historia inasema mtu wa kwanza kuzuru kaburi la mtukufu huyo alikuwa Sahaba wa Mtume Muhammad (saw) Jabir bin Abdillah al Ansari ambaye alifika Karbala na kwenye kaburi la Imam Hussein katika siku ya arubaini tangu baada ya mauaji yake.

Tags