Hatua ya Nne ya Iran; Kufeli 'Mashinikizo ya Juu Zaidi' ya Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: 'Marekani ni kinara wa shari, mwanzilishi na muungaji mkono wa ugaidi duniani."
Sayyid Abbas Mousavi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Alhamisi usiku akijibu matamshi ya Morgan Ortagus msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alihoji: "Je, si ni jambo la kushangaza kusikia matamshi hayo, kutoka kwa utawala ambao kwa hakika ni kinara wa shari na sera za upande mmoja duniani, utawala ambao pia ni muungaji mkono wa kifedha wa ugaidi duniani?
Baada ya Iran kuchukua uamuzi wa kuanza kutekeleza hatua yake ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, kufuatia hatua ya Marekani kukiuka mapatano hayo, Morgan Ortagus ametoa matamshi yaliyojaa chuki dhidi ya Iran na kudai kuwa Iran inatumia vibaya kadhia ya nyuklia na ameitaka jamii ya kimataifa iongeze mashinikizo dhidi ya Iran.
Matamshi hayo yanaonyesha kuwa, sera za 'Mashinikizo ya Juu Zaidi' ambazo zimekuwa zikitekelezwa na Marekani dhidi ya Iran zimefeli na sasa watawala wa Washington wanataka dunia ichukue hatua dhidi ya Iran.
Baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 2018, na baada ya hapo kuanza kutekeleza sera za 'Mashinikizo ya Juu Zaidi' dhidi ya Iran, bado haijaweza kufikia malengo yake kwani taifa la Iran nalo linatekeleza sera ya 'Muqawama au Mapambano ya Juu Zaidi' katika kukabiliana na utumiaji mabavu na sera za upande mmoja za Marekani. Sera ambazo Iran inazifuata zimepelekea kusambaratika mashinikizo hayo ya juu zaidi ya Marekani dhidi yake.
Kwa maneneo mengine tunaweza kusema kuwa, sera za Marekani za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran zimefeli na hivyo kupelekea Washington itengwe zaidi duniani. Dalili ya nukta hiyo ni msimamo wa Marekani baada ya Iran kuchukua hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA.
Ripoti za hivi karibuni za Mfuko wa Kimataifa wa Fedha na Benki ya Dunia zimebaini kuwa, uchumi wa Iran unaelekea katika ustawi na kwamba uchumi huo sasa hautegemei tena pato la uuzaji mafuta ghafi ya petroli. Hiyo ni dalili ya wazi ya kufeli vikwazo na sera za upande mmoja za Marekani dhidi ya Iran. Kutenganisha pato la mafuta na uchumi ni dalili ya namna Iran ilivyo na vyanzo vingi vya mapato katika uchumi wake na jambo hilo limepelekea uchumi wa Jamhuri ya Kiislamu uchukue mkondo wa ustawi.
Kuhusiana na nukta hiyo, jarida la Kimarekani la Foreign Affairs siku ya Alhamisi katika makala baada ya Iran kuchukua hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji katika mapatano ya JCPOA liliandika kuwa: "Iran imeweza kuvuka vikwazo vya Marekani kwa mafanikio na inaendelea na shughuli zake za nyuklia na pia ushawishi wake katika eneo unaimarika."
Huko nyuma Wamarekani walikuwa wamedai kuwa, mashinikizo yao ya juu zaidi na vitisho ni nukta mbili ambazo zitapelekea Iran kupunguza shughuli zake za nyuklia na ushawishi katika eneo la Asia Magharibi.
Hatua ya Nne ya Iran kupunguza uwajibikaji katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA imeonyesha kuwa, ustawi wa shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani, haziwezi kusimamishwa kwa vikwazo na mashinikizo ya Marekani na jambo hilo linaashiria nukta hii muhimu kuwa, teknolojia hasa teknolojia ya nyuklia nchini Iran sasa inategemea wasomi wa ndani ya nchi pasina kuwepo msaada wa kigeni.
Sambamba na kufuata sera yake ya maamuzi ya upande mmoja, Marekani pia inatoa vitisho na kueneza wahaka katika nchi zingine ili zifuate sera zake dhidi ya Iran na hili limeonekana wazi katika kadhia ya JCPOA baada ya washington kujiondoa.
Kuhusiana na hilo, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia siku ya Alhamisi alisema hatua ya Iran kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA ni matokeo ya sera za Marekani. Aliongeza kuwa: 'Si tu kuwa Marekani inakiuka ahadi zake za kimataifa, bali pia kwa vitisho vya adhabu kupitia vikwazo, inazizuia nchi zingine kutekeleza mapatano ya JCPOA.'
Maamuzi ambayo Iran imeyachukua kuhusu JCPOA ni ya haki na yaliyotarajiwa katika kujibu mwenendo usio sahihi wa Marekani na nchi za Ulaya.
Hivyo Iran haitumii vibaya kadhia ya nyuklia kama inavyodai Marekani bali ni Marekani yenyewe ndiyo ambayo kwa kuweka masharti, vitisho na kueneza wahka inafuatilia kimabavu maslahi yake dhidi ya Iran.