Rais Rouhani: Palestina na Quds ndiyo maudhui kuu ya Umma wa Kiislamu
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa Palestina na Quds tukufu ndiyo maudhui kuu ya Umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Ulimwengu wa Kiislamu hautawaruhusu maadui kuwafanya walimwengu wasahau kadhia ya Palestina na Quds tukufu.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran. Ameashiria kufeli kwa siasa za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mwamko na kuwa macho ulimwengu wa Kiislamu na kusema: Mauaji ya raia madhlumu wa Afghanistan, mauaji ya watu wa Iraq na raia wanaodhulumiwa wa Yemen, na kuzusha hitilafu na mifarakano katika nchi za Waislamu ni baadhi tu ya matokeo ya njama habithi za Marekani katika eneo hili.
Rais Rouhani amesisitiza kuwa Palestina inapaswa kukombolewa na Wapalestina na Waislamu shupavu na kuongeza kuwa: Kizazi cha vijana kinapaswa kutambua kuwa, Marekani sio na haiwezi kuwa rafiki wa mataifa ya eneo hili na Waislamu; hivyo masuala ya kieneo yanapaswa kutatulia na wakazi wake.
Rais wa Iran ameeleza masikitiko yake kutokana na mwenendo wa baadhi ya nchi za Waislamu wa kufanya mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kutumia suhula za kijasusi za utawala huo dhidi ya mataifa ya Waislamu na kambi ya mapambano. Amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko katika safu ya mbele ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani katika kuwatetea watu wa Palestina.
Mkutano wa 33 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza leo Alkhamisi hapa mjini Tehran kwa kaulimbiu ya "Umoja wa Umma wa Kiislamu katika Kulinda Msikiti wa al Aqsa". Mkutano huo unaohudhuriwa na wasomi, wanasiasa, wahadhiri wa vyuo vikuu na wanafikra 400 kutoka nchi 90 duniani, utaendelea hadi Jumamosi ijayo.