Zarif azungumza na Haniya, asema Iran imesimama pamoja na taifa la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57356-zarif_azungumza_na_haniya_asema_iran_imesimama_pamoja_na_taifa_la_palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amefanya mazungumzo na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, na kumpongeza kufuatia ushindi wa wanamuqawama (wanamapambano) wa Palestina mbele ya utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko pamoja na taifa la Palestina na inasimama pamoja na wanamapambano shujaa katika Ukanda wa Ghaza."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2019 01:25 UTC
  • Zarif azungumza na Haniya, asema Iran imesimama pamoja na taifa la Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amefanya mazungumzo na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, na kumpongeza kufuatia ushindi wa wanamuqawama (wanamapambano) wa Palestina mbele ya utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko pamoja na taifa la Palestina na inasimama pamoja na wanamapambano shujaa katika Ukanda wa Ghaza."

Katika mazungumzo ya simu na Haniya, Zarif ameongeza kuwa, sababu za ushindi wa Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza wakati wa kukabiliana na Wazayuni maghasibu ni nguvu za wanampambano na umoja wao pamoja na uzingatiaji maadili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha masikitiko yake kutokana na Umoja wa Mataifa kushindwa kuchukua hatua za kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na kusema: "Kutokana na mashinikizo ya Marekani, Umoja wa Mataifa haujaweza kutekeleza majukumu yake."

Katika mazungumzo hayo, Ismail Haniya  amemshukuru Zarif kwa kumpigia simu na pia ametoa shukrani zake za dhati kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuendelea kuunga mkono harakati za muqawama na ukombozi wa Palestina.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hama aidha amesema Wazayuni maghasibu kamwe hawataweza kufikia malengo yao katika Ukanda wa Ghaza.

Ziyad al-Nakhalah Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina

Siku ya Jumapili pia Zarif alimpigia simu Ziyad al-Nakhalah Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina ambapo sambamba na kulaani hujuma mpya ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza, amewapongeza wanamapambano wa Palestina kwa kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukubali usitishwaji vita. Kwa siku mbili mfululizo kuanzia Jumanne iliyopita, utawala wa Kizayuni ulitekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya Ukanda wa Ghaza ambapo Wapalestina 34 waliuawa shahidi na wengine 100 kujeruhiwa. Katika kujibu mashambulizi hayo, wanamapambano wa Palestina walivurumisha maroketi zaidi ya 400 katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Kufuatia jibu hilo kali, utawala wa Kizayuni ulisalimu amri na kulazimika kuomba usitishwaji vita kuanzia Alhamisi asubuhi. Hatua hiyo imetathminiwa kuwa ni ushindi kwa wapigania ukombozi wa Palestina.

Tokea mwaka 2006, Ukanda wa Ghaza uko chini ya mzingiro wa kinyama wa nchi kavu, angani, na baharini ambao unatekelezwa na utawala haramu wa Israel na hivyo kuwasababishia matatizo makubwa Wapalestina wa eneo hilo.