Araqchi: Kubakia hai JCPOA kutategemea jitihada za EU
(last modified Sat, 30 Nov 2019 04:29:56 GMT )
Nov 30, 2019 04:29 UTC
  • Araqchi: Kubakia hai JCPOA kutategemea jitihada za EU

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema kuyanusuru na kuyabakisha hai makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kutategemea na jitihada za Umoja wa Ulaya na kutekeleza kwao majukumu yao kwa mujibu wa mapatano hayo.

Sayyid Abbas Araqchi amesema hayo katika mahojiano na gazeti la Ujerumani la NCR ambapo amefafanua kuwa, "Kuna matumaini bado ya kuyanusuru makubaliano hayo, lakini hilo litategemea namna nchi za Ulaya zitakavyofungamana na makubaliano hayo ya kimataifa."

Amebainisha kuwa, JCPOA kwa sasa ipo katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), na nchi za Ulaya hazina budi kufanya juu chini ili kuinusuru.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amebainisha kuwa, "Jambo moja ambalo Iran imejifunza hadi sasa ni kuwa, kufikiwa makubaliano ya nyuklia na madola yenye nguvu duniani kumepelekea taifa la Iran likabiliwe na vikwazo zaidi, na sio kinyume chake kama ilivyotarajiwa."

Amesema iwapo mwenendo huu wa vikwazo utaendelea, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italazimika kubadilisha mtazamo na mwelekeo wake na kuongeza kwamba, "Jambo jingine ambalo tumejifunza kama taifa, ni kuwa muqawama na mapambano ni bora kuliko ushirikiano."

Mei 2018, Trump aliiondoa Marekani kwenye JCPOA na kushadidisha vikwazo dhidi ya Iran

Sayyid Araqchi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kutumia vipengee vya 26 na 36 vya JCPOA vinavyosema kuwa, iwapo upande wa pili hautafungamana na ahadi zake katika mapatano hayo, Iran ina haki ya kusitisha kwa ujumla au hatua kwa hatua utekelezaji wa ahadi zake.

Novemba 6 Iran ilichukua hatua yake ya nne ya kuounguza utekelezaji wa ahadi zake katika JCPOA na imefanya hivyo baada ya nchi tatu za Umoja wa Ulaya ambazo zilitia saini mapatano ya JCPOA kushindwa kuchukua hatua yoyote ya kivitendo kukabiliana na vitisho na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Tags