Kiongozi Muadhamu atoa amri ya kufanyika uchunguzi wa mkasa wa kuanguka ndege
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza masikitiko yake kuhusiana na mkasa wa ndege ya abiria ya Ukraine iliyotunguliwa kimakosa karibu na mji wa Tehran ambapo sambamba na kusema kuwa, yuko pamoja na familia zilizopoteza ndugu zao katika mkasa huo wa kuhuzunisha ametoa amri ya kufanyika uchunguzi kuhusiana na uwezekano wa kufanyika uzembe na wahusika kuchukuliwa hatua.
Ayatullah Ali Khamenei amesema katika ujumbe wake huo: Ninasisitiza kwamba, kuna haja ya kufanyika uchunguzi wa tukio hilo chungu na kuchukuliwa hatua za maana kuhakikisha kwamba, hakujitokezi tena tukio kama hili.
Mwishoni mwa ujumbe wake huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaombea rehema na maghufira waliopoteza maisha katika mkasa huo wa kuangushwa kimakosa ndege ya abiria ya Ukraine na kuzitakia familia zao subira na ujira mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wakati huo huo mapema leo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kosa la kibinadamu lililotokana na vitisho vya Marekani vya kushambulia maeneo nyeti nchini Iran ndiyo sababu ya kuanguka ndege ya abiria ya Ukraine karibu na Tehran.
Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Iran imetoa taarifa rasmi ikiashiria vitisho vya Rais wa Marekani na majenerali wa jeshi la nchi hiyo vya kushambulia maeneo kadhaa muhimu ndani ya ardhi ya Iran sambamba na kuongezeka ndege za kijeshi za magaidi wa Marekani zilizokuwa zinaruka wakati huo karibu na Iran na kusema: Katika mazingira kama hayo, kulitokea kosa la kibinadamu lililopelekea kutunguliwa ndege hiyo baada ya kukaribia sana katika kituo kimoja nyeti cha kijeshi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.