Zarif aziasa nchi za Ulaya kusimama kidete mkabala wa vitisho vya Trump
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema hatua ya Marekani ya kutoa vitisho vipya vya kuziwekea nchi za Ulaya ushuru mpya wa kibishara inadhihirisha kuwa, kutumbukia nchi za EU kwenye mtego wa Rais Donald Trump kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kumekuwa na maslahi zaidi kwa kiongozi huyo wa Marekani na sio kwa nchi hizo za Ulaya.
Mohammad Javad Zarif amezikosoa nchi za Ulaya kwa kujidhalilisha mbele ya Marekani katika ujumbe alioutuma leo Jumatano kwenye ukurasa wake wa Twitter, ulioambatanishwa na ripoti iliyoko kwenye gazeti la Washington Post ambayo imeashiria vitisho vipya vya Trump dhidi ya Ulaya akiwa katika Jukwaa la Uchumi Duniani mjini Davos jana Jumanne.
Katika ujumbe huo, Dakta Zarif amezihutubu nvhi za Ulaya kwa kusema,"Samahani kusema nilikuambieni hivi: Wakati E3 (Uingereza, Ujerumani na Ufaransa) zilipouza mabaki ya JCPOA ili kuepuka ushuru wa Trump wiki iliyopita, nilizionya kuwa (hatua hiyo haitakuwa na tija nyingine ghairi ya) kuzidisha hamu ya Trump."
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa, licha ya nchi za Ulaya kuuza heshima zao, lakini Trump ametishia tena kuziwekea ushuru mpya. Trump amesema serikali yake itaziwekea nchi za Ulaya ushuru mpya wa asilimia 25 kwa magari ya nchi hizo yanayouzwa Marekani.
Hivi karibuni, nchi tatu za Troika ya Ulaya yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa ziliamua kuanzisha mchakato wa kutatua hitilafu ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA unaofahamika kama "Trigger Mechanism" kwa madai kuwa Iran imepunguza uwajibikaji wake kwenye mapatano hayo ya kimataifa, lakini ilibainika kuwa walichukua hatua hiyo kwa mashinikizo ya Trump.
Hii ni katika hali ambayo, Iran iliamua kuchukua hatua tano za kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA, kufuatia nchi za Ulaya kushindwa kudhamini maslahi ya Iran kwenye makubaliano hayo baada ya Marekani kujiondoa kwayo.