Woga wa nchi za Ulaya wa kukabiliana na ubeberu wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58777-woga_wa_nchi_za_ulaya_wa_kukabiliana_na_ubeberu_wa_marekani
Dakta Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la kila wiki la Der Spiegel la nchini Ujerumani kwamba kitendo cha nchi za Ulaya cha kutii kibubusa amri za Marekani ni janga na maafa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 27, 2020 07:36 UTC
  • Woga wa nchi za Ulaya wa kukabiliana na ubeberu wa Marekani

Dakta Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la kila wiki la Der Spiegel la nchini Ujerumani kwamba kitendo cha nchi za Ulaya cha kutii kibubusa amri za Marekani ni janga na maafa.

Katika mahojiano hayo Dakta Zarif aliashiria pia uwezekano wa nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wa kutumia Mchakato wa Kutatua Hitilafu ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA kuishinikiza Iran na kubainisha kwamba, madola hayo hayana hoja za kisheria za kutumia mchakato kama huo.

Mchakato wa Kutatua Hitilafu ni hatua ya mwisho iliyoainishwa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya kutatua hitilafu zinazojitokeza katika makubaliano hayo na inaweza kuishia kwenye kurejeshewa Iran vikwazo vilivyoondolewa baada ya kufikiwa mapatano hayo. Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema, nchi za Russia na China zina mtazamo mmoja na Tehran kuhusu suala hilo.

Nchi za Ulaya zinadai kuwa zimeamua kuanzisha mchakato huo ili kuilazimisha Tehran irejee kwenye ahadi zake, wakati ambapo huko nyuma Iran ilikuwa imezipa nchi za Ulaya muda wa mwaka mzima kuchukua hatua za kivitendo za kuheshimu mapatano ya JCPOA na kutekeleza ahadi zao lakini zimeshindwa kuheshimu makubaliano hayo kwa kuiogopa Marekani. Ni jambo lililo wazi kwamba, Tehran haikubakishiwa njia nyingine isipokuwa kuchukua hatua mkabala wa kitendo cha Marekani cha kujitoa bila ya sababu katika makubaliano hayo yenye baraka kamili za Umoja wa Mataifa na ndio maana Tehran imeamua kupunguza ahadi zake kwa awamu tano ndani ya JCPOA huku ikisisitiza kuwa, misimamo yake kuhusu mapatano hayo haijabadilika na wakati wowote ule nchi za Ulaya zitakapoanza kuheshimu na kutekeleza kivitendo ahadi zao ndani ya JCPOA, basi Tehran nayo itarejea kama ilivyokuwa zamani. 

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA

 

Kwa mara kadhaa huko nyuma, nchi za Ulaya zilikuwa zinakiri kwamba Tehran imeheshimu kikamilifu ahadi zake ndani ya JCPOA. Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA ambao ndiye msimamizi wa utekelezaji wa makublaiano hayo, umetoa ripoti zapata 16 kuthibitisha kuwa Iran imeheshimu kikamilifu ahadi zake ndani ya JCPOA. 

Amma tukirejea katika hatua ya nchi za Ulaya ya kuanzisha mchakato wa kutatua hitilafu ndani ya JCPOA, ukweli ni kuwa, nchi hizo zina wasiwasi mkubwa wa madhara ya hatua yao hiyo na zinaogopa hatua zitakazochukuliwa na Iran kujibu kitendo chao hicho. Ndio maana hivi sasa nchi hizo zimeamua kuikabidhi kamati ya pamoja ya JCPOA kulifuatilia suala hilo.  

Abdul Reza Farrokhi Zadeh, mhadhiri wa chuo kikuu na mtaalamu wa jeopolitiki anaamini kuwa, hatua ya nchi za Ulaya ya kuanzisha Mchakato wa Kutatua Hitilafu haina maana ya kulirejesha suala la nyuklia la Iran kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wala kuirejeshea vikwazo Iran, bali nchi za Ulaya zinataka kuanzisha mazungumzo mapya na Tehran, tab'an mazungumzo yaliyoambatana na vitisho ili kuiweka Iran chini ya mashinikizo.

Matamshi ya Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza wakati alipohojiwa na televisheni ya BBC ya kwamba inabidi makubaliano ya JCPOA yafutwe na sehemu yake iwekwa "Makubaliano ya Trump" ni ushahidi wa wazi wa suala hilo.

Dakta Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alipohojiwa na gazeti la kila wiki la Der Spiegel la Ujerumani

 

Hata hivyo hivi sasa nchi za Ulaya ziko njia panda, hazijui ziendelee na mapatano ya JCPOA au ziifuate Marekani iliyojitoa katika makubaliano hayo. Nchi hizo zina wasiwasi kuhusu majibu yatakayotolewa na Iran iwapo zitajitoa. Tab'an Iran imethibitisha kivitendo kuwa inaheshimu sheria kikamilifu katika majibu yake na kamwe haiwezi kuchukua hatua zilizo kinyume cha sheria. Muda wote Tehran imekuwa ikisisitiza kuwa, italinda haki zake kwa nguvu zake zote, lakini kwa mujibu wa sheria zilizopo. 

Ndio maana pia wakati akijibu swali kuhusiana na tishio la Iran la kujitoa katika Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), waziri Zarif alisema katika mahojiano yake hayo na gazeti la Der Spiegel la Ujerumani kwamba, kama Iran itajitoa katika mkataba huo haitakuwa na maana ya kutaka kuunda bomu la nyuklia. Iran haina mpango kabisa wa kuunda bomu kama hilo kwani jambo hilo linakinzana na misingi ya kimaadili na kiitikadi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Dakta Zarif aliashiria pia jinai ya Marekani ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kusema kuwa, Marekani, Ulaya na jamii ya kimataifa ina deni kwa shahidi Qassim Soleimani kutokana na mchango wake mkubwa uliopelekea kuangamizwa genge la kigaidi la Daesh katika eneo hili na kwamba wananchi wa Asia Magharibi ndio watakaotoa majibu makali kwa Marekani kutokana na jinai yake ya kumuua kigaidi shujaa huyo.